Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Mganga Mkuu wa jiji la Mbeya Dkt Samuel Lazaro.
Na Mwandishi wetu,

ZOEZI la utoaji chanjo  ya Surua Rubella, minyoo na kichocho  kwa watoto na watu wazima, Mkoani Mbeya, huenda lisifikie malengo yake kutokana na shule binafsi za Msingi na Sekondari, kudaiwa  kutoa ushirikiano hafifu kwa serikali kwa kile kinachodaiwa kuhofia wazazi kuwaondoa watoto wao.

Akizungumzia hilo, Mganga Mkuu wa halmashauri ya Jijiji la Mbeya, Samweli Lazaro, alisema huenda zoezi hilo lisifanikiwe kwa aslimia 100 kutokana na ugumu uliopo  wakati wa utoaji huduma hiyo kwa watoto walio shuleni hususani  katika shule zinazomilikiwa na watu binafsi.

Amesema, lengo la serikali kwa Jiji la Mbeya, nikufikia watoto na watu wazima  630324 ambao watapatiwa chanjo ya Surua Rubella, dawa za minyo, matone ya vitamini A na dawa zinazokinga Usubi, minyoo ya Tumbo, Matende na Mabusha kwa kuzingatia makundi yao.

Amesema, ugumu unakuja kwa kundi la watoto walio katika umri wa miaka 5 hadi 18 ambao asilimia kubwa ni wanafunzi  na hasa wanaopata elimu katika shule za binafsi.

Amesema, hali hiyo inatokana  na kasumbua walioyokuwa nayo baadhi ya wazazi baada ya tukio la Morogoro kutokea la watoto 363 kupoteza fahamu mwaka 2008  baada ya kupewa dawa ya minyoo na kichocho.

Amesema, hivyo kasumbua hiyo bado imewakaa baadhi ya wazazi jambo linalowapa ugumu walimu wa shule hizo za binafsi kuruhusu watoto kupatiwa huduma hiyo kwa kigezo kwamba ni lazima wazazi watoe kibali jambo ambalo ni changamoto kubwa kwa serikali kutimiza malengo yake.

“Utafiti unaonyesha kwamba walimu au wamiliki wa shule wamekuwa wakitoa ushirikiano hafifu kwa serikali katika zoezi hili la utoaji wa chanjo na dawa mbalimbali  kwa wanafunzi walio shuleni kwa kuhofia wazazi kuwaondoa watoto wao hivyo kuathirika kiuchumi,”alisema.

Amesema, shule binafsi zimekuwa zikijiendesha kupitia ada zinazotolewa na wazazi hivyo shule ikikumbwa na skendo hiyo basi hupoteza sifa hivyo  kusababisha jamii kutoandikisha wanafunzi katika shule hiyo.

Aidha,  Dkt. Lazaro aliwaomba walimu pamoja na wazazi kuondokana na mtazamo huo kwani kinachotakiwa kufanyika ni kutoa elimu kwa jamii ili kutambua umuhimu wa chanjo na dawa hizo katika mwili wa mwanadamu.

Watoto 171,862 walio katika umri wa miezi 9 mpaka chini ya miaka 15 wanatarajia kupata chanzo ya Surua Rubella, 62772 wenye umri wa miezi 6 mpaka miezi 59 wanatarajia kupewa matone ya vitamin A, dawa za minyoo watoto  miezi 12 hadi 59 huku watoto kati ya miaka 5 na kuendelea 345,110 watapatiwa dawa zinazokinga Usubi, Minyoo ya Tumbo, matende na mabusha.

Mwisho.

Je, Una Habari,Picha,Tangazo,Makala, Ushauri n.k.?Basi Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp 0759 406 070

Post a Comment

 
Top