Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Na EmanuelMadafa,Mbeya
MAHAKAMA ya Wilaya ya Chunya, Mkoani Mbeya, imetoa kibali cha kukamatwa na kuuzwa kwa magari matatu  ya Taasisi ya Kibenki ya NMB na  Kampuni ya mawasiliano Vodacom Tanzania, ili kulipa fidia ya shilingi milioni 86,553,700 kwa kosa la kumsababishia mteja hasara baada ya kuhamisha fedha kwenye akaunti kwa kutumia huduma ya  kibenki  ya njia ya simu bila idhini yake.

Kesi hiyo namba 4 imefunguliwa mahakamani hapo, Mei 13 mwaka huu na mlalamikaji Mwanswa Jonas dhidi ya Taasisi ya kibenki ya NMB na kampuni ya Vodacom Tanzania  na mahakama hiyo kutoa hukumu Oktoba 13 mwaka huu kwa kutoa kibali cha kuuzwa kwa magari hayo.

Akisoma shitaka hilo, hivi karibuni, Kalani wa mahakama ya Wilaya ya Chunya Izza Sheumu, mbele ya hakimu wa Wilaya, Desdery Magezi, alisema, Mei 13,2014 , mlalamikaji alibaini kupotea kwa fedha zake zikiwa na thamani ya shilingi milioni 6,553,700 zilizokuwa kwenye akaunti namba 6071600335 kupitia benki ya NMB.

Amesema, uchunguzi ulibaini kuwa fedha hizo zilipotea baada ya kuhamishwa kwa kutumia huduma ya kibenki ya njia ya simu kutoka akaunti namba 6071600335 kwenda kwenye namba ya simu  ya mkononi ya Vodocom 0768 713668 bila ya idhini ya mteja.

Amesema, imeelezwa kuwa wakati zoezi hilo linafanyika mteja huyo alisitishiwa huduma ya mawasiliano kwa muda na kwamba alipofuatilia kwenye ofisi za Vodacom, alielezwa kwamba asubiri huduma yake itarudishwa kwani kunamatatizo ya kiufundi.

Amesema, mlalamikaji  huyo akiwa katika harakati za kuweka kiasi cha fedha cha shilingi milioni 16 kupitia kwenye akaunti yake iliyopo katika benki ya NMB kabla ya kuweka fedha hizo aliomba salio na kuambia salio lake halitoshi licha ya akaunti yake kudaiwa kuwa na kiasi cha fedha  zaidi ya shilingi milioni sita.

Amesema, alipofuatilia alishangazwa kuelezwa kwamba fedha hizo alizitoa yeye kupitia namba yake ya simu ya mkononi ya Vodocom jambo ambalo alilipinga hivyo kuamua kupeleka malalamiko yake kwenye ofisi za wanasheria Tanganyika Law Society na kesi hiyo kusimamiwa na wakili wa kujitegemea, Radlsaus Lwekaza, ambaye aliiomba mahakama kusikiliza kesi hiyo, Julai 24, mwaka huu.

Pia, imeelezwa kuwa wakili, Rwekeza, aliiomba mahakama kusikiliza kesi hiyo upande mmoja, kwa kuelezea kwamba wadaiwa wameamua kwa makusudi kutohudhuria na kujitetea kwenye kesi husika baada ya mahakama kuhairisha kesi hiyo mara nyingi bila ya wao kutokea licha ya kupelekewa hati ya kuitwa.

Amesema, baada ya hapo kesi ilisikilizwa upande mmoja,  na mahakama hiyo kutoa hukumu 15/8/2014 ya kwamba mshitakiwa namba moja ambaye ni NMB alipe shilingi milioni 43, 272,750 na Vodacom alipe milioni 43,272,750 ambapo mdai aliomba kukazia hukumu baada ya siku 30 za rufaa kupita na mahakama ilimkubalia na hatimaye Oktoba 13 mwaka huu mahakama ilitoa kibali kwamba magari mali ya NMB na Vodacom kuuzwa.

Mahakama hiyo, iliyataja magari hayo kuwa ni gari namba T519 CHP Nissan Patrol nyeupe , T947 CVE Toyota Land Cruiser mali ya Taasisi ya Kibenki ya NMB na gari namba T388 CGW Nissan Hard Bord mali ya kampuni ya Vodocom.

Aidha, mahakama hiyo ilitoa kibali kwa Kampuni ya Jagro Enterprices limited, inayomilikiwa na Maulid Hamis kukamata magari hayo.


Mwisho.

Je, Una Habari,Picha,Tangazo,Makala, Ushauri n.k.?Basi Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp 0759 406 070

Post a Comment

 
Top