Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This



Na Emanuel Madafa,mbeya

KUTOKANA na  mkondo wa hali ya hewa uliombata maji maji  unaotoka nchini Congo, kuvamia anga la Mkoa wa Mbeya na kusababisha hali mbaya ya hewa , leo  ndege ya Fastjet  imeshindwa kutua na kulazimika kurejea Jijini Dar es Salaam.

Mkondo huo wa hewa , umetajwa kuvamia eneo la uwanja huo dakika 30  kabla ya ndege kutua katika uwanja wa Songwe, hali iliyosababisha rubani wa ndege kuuzunguka uwanja huo zaidi ya mara mbili na mwishowe kurejea tena Jijini Dar es Saalam.

Akizungumzia tatizo hilo, Meneja Mamlaka ya hali ya hewa Nyanda za Juu Kusini, Issa Mohamed, alisema saa moja kabla ya ndege hiyo kutua hali ya hewa ilikuwa vizuri, tatizo limejitokeza ndani ya nusu saa baada ya mkondo huo wa hewa uliombatana na  maji maji unaotokea nchini Congo kuvamia eneo la  uwanja wa  ndege wa Songwe na kusababisha hali ya hewa kuchafuka.

Amesema, Mkoa wa Mbeya upo karibu na misitu ya Congo hivyo baada ya hali hiyo kuvamia  asubuhi ilikutana na  mambonde na tabaka la  chini likiwa na  ubaridi  kuliko hali yenyewe ya kawaida ndani ya nusu saa kabla ya ndege hiyo kutua.


Aidha, amesema tatizo hilo haliwezi kutatuliwa kwani ni mabadiliko ya hali ya hewa, jambo linalotakiwa kufanywa na mamlaka ya ndege ni (TIAA) inaweka taa za muda  ambazo humwezesha rubani kutambua njia sahii wakati anatua hata kama hali ya hewa itakuwa mbaya.


Naye, Mratibu wa shughuli za ndege kutoka Kampuni ya Fastjet Mkoa wa Mbeya, Omary Idrisa, amesema ndege hiyo imeshindwa kutua kutokana na hali ya hewa kuwa mbaya hivyo kulazimika kugeuza Jijini Dar es Salaam ikiwa na zaidi ya abiria 100.

Amesema   kwamba ndege hiyo  ilitakiwa kutua saa mbili asubuhi na dakika 25 na kuruka saa tatu na dakika tano, ikatua leo majira ya saa tisa mchana na kuondoka saa 11 za jioni kwa mujibu wa taarifa kutoka mamlaka ya hali ya hewa.

Meneja wa Uwanja wa Ndege wa Songwe, Valentine Kadeha, alikiri ndege hiyo kushindwa kutua kwenye  uwanja huo, hivyo kulazimika kugeuza Jijini Dar es Salaam kutokana na hali ya hewa kuwa mbaya.


Hii ni mara ya pili ya ndege ya Fastjet kushindwa kutua katika kipindi cha wiki tatu ndani ya mwezi huu wa January 2015.
MWISHO



Je, Una Habari,Picha,Tangazo,Makala, Ushauri n.k.?Basi Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp 0759 406 070

Post a Comment

 
Top