Waziri
wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, akizungumza na
Wakurugenzi wa Bodi mpya ya Wakala wa Nishati Vijijini - REA (hawapo
pichani), wakati alipokuwa akiizindua rasmi Bodi hiyo Makao Makuu ya
Wizara mjini Dodoma, Aprili 19, 2017.
Na Veronica Simba – Dodoma
Waziri
wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo, amezindua Bodi mpya ya
Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na kuiagiza kufanya kazi kwa
kutanguliza maslahi ya Taifa na Watanzania kwa ujumla.
Profesa Muhongo alizindua Bodi hiyo jana, Aprili 19, 2017 Makao Makuu ya Wizara mjini Dodoma.
Akizungumza
na Wakurugenzi wa Bodi hiyo mpya, wakati wa hafla ya uzinduzi, Profesa
Muhongo aliwaagiza kuhakikisha wanawasimamia wakandarasi waliochaguliwa
kutekeleza miradi ya umeme vijijini ili wanunue vitendea kazi ikiwemo
nguzo, transfoma na nyaya za umeme kutoka kwa wazalishaji wa ndani ya
nchi.
“Wakandarasi
ni lazima wanunue vifaa hivyo ndani ya nchi. Vikiisha hapa nchini,
ndiyo waagize nje. Hatutavumilia kuona mkandarasi ananunua vitendea kazi
nje ya nchi wakati hapa nchini vipo tele.”
Hata
hivyo, Profesa Muhongo alisisitiza suala la ubora ambapo alifafanua
kuwa, ni lazima vitendea kazi vinavyonunuliwa viwe katika ubora
unaostahili. “Japokuwa tunataka vitu kutoka ndani ya nchi lakini ni
lazima tuzingatie suala la ubora wake.”
Akiendelea
kutoa maagizo kwa Bodi hiyo, Waziri Muhongo pia alielekeza kwamba,
Kampuni zote za kigeni ambazo zimeshinda Tenda ya kutekeleza miradi ya
umeme vijijini awamu ya Tatu (REA III), ni lazima zifanye kazi na
wakandarasi wadogo (sub-contractors) wa kitanzania.
“Ni
lazima wakandarasi wadogo wote watoke Kampuni za Kitanzania. Inaweza
kuwa Kampuni iko hapa nchini lakini siyo ya watanzania; hiyo hatuitaki.
Mradi huu unalenga kuwawezesha watanzania hivyo ni lazima wapate fursa,”
alisisitiza Waziri.
Profesa
Muhongo alitumia fursa hiyo kuhamasisha watanzania wenye sifa
kujitokeza kwa wingi ili wafanye kazi na kampuni kubwa za wakandarasi
kutoka nje, na baadaye waweze kujitegemea na kujenga uwezo wa kufanya
kazi hizo wao wenyewe.
Aliiagiza
Bodi hiyo kuhakikisha wanatatua changamoto ya baadhi ya vibarua
kutokulipwa malipo yao baada ya kufanya kazi. Aliwataka kuweka usimamizi
utakaowezesha kila mmoja kulipwa stahili zake kulingana na kazi
aliyofanya.
Vilevile,
Profesa Muhongo aliitaka Bodi kusimamia ubora wa kazi inayofanywa na
wakandarasi husika kwani kutokana na uzoefu inaonesha kwamba, baadhi
yao, kazi zao hazina ubora unaoridhisha.
Alisema,
Bodi inawajibika kumfuatilia kila Mkandarasi kujiridhisha kuhusu uwezo
wake, hata kama ameshapitishwa na taratibu za manunuzi. Alisema, endapo
Bodi itakuwa na wasiwasi na uwezo wa Mkandarasi, ni lazima iweke hilo
wazi kwani kazi isipofanyika ipasavyo, hawatakwepa lawama.
“Iteni
kampuni moja baada ya nyingine mjiridhishe na utendaji wao. Muone eneo
alilopewa, ukubwa wa eneo hilo na bajeti aliyopewa. Pia mumuulize kuhusu
vitendea kazi alivyonavyo pamoja na wataalam alionao,” alisisitiza.
Aidha,
Profesa Muhongo aliwataka wakurugenzi wa Bodi hiyo kujenga utaratibu wa
kutembelea maeneo inakotekelezwa miradi mbalimbali ya umeme vijijini
ili kujionea kwa macho maendeleo ya kazi inayofanyika.
Suala
jingine muhimu ambalo Waziri aliwaelekeza wakurugenzi wa Bodi
kulifanyia kazi, ni kupitia taarifa ya utekelezaji wa REA II ili pamoja
na mambo mengine, waweze kujiridhisha na majina ya wakandarasi
waliopitishwa kutekeleza REA III. Aliwataka kumkataa Mkandarasi ambaye
watabaini amepewa Tenda kutekeleza REA III wakati alishindwa kazi REA
II.
Pia,
Waziri Muhongo aliitaka Bodi kuwafuatilia wakandarasi husika ili
kuhakikisha wakati wanasambaza umeme vijijini katika awamu hii ya Tatu,
wanatoa kipaumbele kwa maeneo muhimu ikiwa ni pamoja na Taasisi za jamii
kama vile shule, ofisi mbalimbali za uongozi, nyumba za kuabudu, sehemu
za biashara na uzalishaji. “Watu wa mashambani wasiwe wanakuja wizarani
kuomba umeme. Umeme upelekwe kwenye mashamba na hata kwenye Ranchi
mbalimbali. Hatutaki kusikia mtu anarukwa,” alisisitiza.
Sambamba
na maelekezo hayo yote, Profesa Muhongo pia aliitaka Bodi husika,
katika kikao chake cha kwanza, ijadili na kupendekeza namna ya kuongeza
asilimia ya watanzania wenye fursa ya kupata umeme, kutoka ile iliyopo
sasa ambayo ni asilimia 49.5.
“Mje na mapendekezo mnataka tufike asilimia ngapi na kwa kutumia mbinu zipi.”
Awali,
akizungumza na wakurugenzi wa Bodi mpya iliyoteuliwa, Kaimu Katibu Mkuu
wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa James Mdoe, aliwataka kufanya
kazi kwa ushirikiano ili kuleta tija kwa Taifa.
Profesa
Mdoe aliwataja wakurugenzi wa Bodi mpya ya REA walioteuliwa kuwa ni
Dkt. Gideon Kaunda ambaye ni Mwenyekiti pamoja na wajumbe Mhandisi
Innocent Luoga, Happiness Mhina, Stella Mandago, Scholastica Jullu,
Amina Chinja, Theobald Sabi na Michael Nyagoga.
Alisema
kuwa, Waziri Muhongo, amefanya uteuzi huo kutokana na Mamlaka
aliyonayo, chini ya Kifungu Namba 5(1) (b) na Namba 8(3) cha Sheria ya
Nishati Vijijini ya mwaka 2005, akiwa ndiye Waziri mwenye dhamana.
Kwa
upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga, kwa
niaba ya Wakala huo, aliahidi kutoa ushirikiano stahiki kwa Bodi
iliyoteuliwa ili kwa pamoja waweze kuleta matokeo chanya katika
kuwapatia umeme wananchi walioko vijijini.
Uteuzi wa Bodi mpya ya REA ni wa miaka mitatu na umeanzia tarehe 1 Aprili, 2017.
Kaimu
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa James Mdoe (kulia),
akiwasomea majukumu yao ya kazi, Wakurugenzi wa Bodi mpya ya Wakala wa
Nishati Vijijini (REA), wakati wa hafla ya uzinduzi rasmi wa Bodi hiyo,
uliofanyika Makao Makuu ya Wizara mjini Dodoma, Aprili 19, 2017.
Mkurugenzi
Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga,
akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Bodi mpya ya REA, uliofanyika
hivi karibuni mjini Dodoma.
Baadhi
ya Wakurugenzi/Wajumbe wa Bodi mpya ya Wakala wa Nishati Vijijini
(REA), wakizungumza mbele ya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa
Sospeter Muhongo (hayupo pichani), wakati wa hafla ya uzinduzi wa Bodi
hiyo uliofanyika hivi karibuni mjini Dodoma.
Waziri
wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (wa tano kutoka kushoto)
akiwa katika picha ya pamoja na Wakurugenzi wa Bodi mpya ya Wakala wa
Nishati Vijijini (REA), mara baada ya kuizindua rasmi hivi karibuni
mjini Dodoma. Kulia kwa Waziri ni Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara, Profesa
James Mdoe na kushoto kwa Waziri ni Mwenyekiti wa Bodi, Dkt. Gideon
Kaunda. Wa kwanza kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Gissima
Nyamo-Hanga.
Waziri
wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kushoto) akiwakabidhi
vitendea kazi, baadhi ya wakurugenzi wa Bodi mpya ya Wakala wa Nishati
Vijijini (REA), wakati wa hafla ya uzinduzi wa Bodi hiyo uliofanyika
mjini Dodoma hivi karibuni.
Baadhi
ya Wakurugenzi wa Bodi mpya ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na
maofisa mbalimbali kutoka wizarani na REA, wakiwa katika hafla ya
uzinduzi wa Bodi hiyo uliofanyika hivi karibuni mjini Dodoma.
Post a Comment