idydc yatoa msaada hospitali iringa

idydc 31 2766c
SHIRIKA lisilo la kiserikali la Iringa Development of Youth Disabled and Children Care (IDYDC) kwa kushirikiana na Redio Nuru FM ya mjini hapa, wametoa misaada ya viti vitano vya kubebea wagonjwa na fimbo 20 za kutembelea kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa. (HM)

Sambamba na kuisadia hospitali hiyo vifaa hivyo vyenye thamani ya sh milioni 3.5, redio hiyo ilivisaidia vituo vya watoto yatima vilivyoko mkoani hapa vya Huruma Center, Sabasaba Center na Kituo cha Wazee Iringa vitu mbalimbali vikiwemo vyakula, vifaa vya usafi, sabuni na mipira kwa watoto hao.
Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo wakitimiza miaka mitatu tangu kuanzishwa kwa kituo hicho, Meneja wa redio hiyo, Victor Chakudika, aliitaka jamii kuwa na moyo wa kujitolea kwa jamii inayoishi katika mazingira magumu.
Alisema lengo la redio hiyo kuwa jirani na jamii inayowahudumia ni kurudisha faida kwa jamii hiyo na itakuwa inafanyika kila mwaka.
Chakudika alisema redio hiyo inatambua umuhimu wa kuchangia huduma za afya, kwani bila wananchi husika kutokuwa na afya njema ina maana hata maendeleo hayatakuwepo.
Muuguzi mfawidhi wa hospitali hiyo, Rustica Tung'ombe kwa niaba ya mganga mkuu, aliishukuru redio hiyo kwa kujali na kuthamini maisha ya Watanzania, kwa kuamini kuwa mchango huo si tu ni kusaidia shughuli za hospitali, bali pia utasaidia kuongeza viti katika hospitali hiyo na kuwasaidia wagonjwa walemavu katika kufanya mazoezi.
Alisema kushirikiana kujenga jamii ya Iringa ni jukumu la kila mwananchi, hivyo vifaa vilivyotolewa vitakuwa faida kwa kila mwanajamii na kuwataka kuendelea kutoa misaada katika hospitali hiyo. Chanzo: Tanzaniadaima

Post a Comment

 
Top