MAMLAKA ya Udhibiti wa
Huduma za Nishati na Maji nchini, EWURA, imeridhishwa na ubora wa mafuta ya
dizeli na petroli yanayouzwa kwenye vituo vya mafuta Wilayani Mbarali mkoani
Mbeya.
EWURA imetoa tathimini
hiyo baada ya ukaguzi uliofanywa na Maafisa wake kwenye vituo vya mafuta
wilayani humo kubaini kuwa vinauza mafuta yasiyochakachuliwa.
Ukaguzi huo unafanyika
kutokana na malalamiko ya madereva wa magari nchini kuwa baadhi ya vituo vya
mafuta vinauza nishati hiyo hasa petrol na dizeli iliyochakachuliwa kwa
kuchanganywa na mafuta ya taa, maji au vimiminika vingine na hivyo kuharibu
injini za magari yao.
Katika ukaguzi huo wa
dharura wilayani Mbarali, Maafisa wa EWURA walikagua vituo vitatu vilivyomo
wilayani humo na kubaini kuwa hakuna mafuta yaliyochakachuliwa yanayouzwa kwa
wateja.
Afisa Ukaguzi wa EWURA,
Raphael Nyamamu, amesema wameridhishwa na hali hiyo inayoonesha kuwa
wafanyabiashara wa mafuta wilayani Mbarali wanafuata sheria za biashara hiyo,
kanuni na taratibu zilizowekwa na EWURA katika uzaaji wa nishati hiyo.
Mmoja kati ya wamiliki
wa vituo vya mafuta wilayani Mbarali, Suleiman Kilemile, amesema wamejifunza
madhara ya kuchakachua mafuta hivyo wapo makini kuhakikisha kuwa hawanunui wala
kuwauzia watu mafuta machafu.
EWURA ipo mkoani Mbeya
kufanya ukaguzi huo kwenye wilaya zote za mkoani hapa ili kuhakikisha sheria,
kanuni na taratibu za uendeshaji wa biashara hiyo zinafuatwa na wafanyabiashara
husika.
Mwisho
Post a Comment