MAHAKAMA ya Mkoa wa Mbeya imewahukumu kifungo cha miaka
30 jela waliokuwa askari wawili, James Kagoma wa Jeshi la Polisi na Juma Mussa
wa Jeshi la Magereza na raia watatu, baada ya kupatikana na hatia katika kesi
ya Unyang’anyi wa Kutumia Silaha.
Mbali na kifungo hicho, mahakama hiyo pia
imeamuru kutaifishwa kwa magari mawili madogo yaliyotumika katika unyang;anyi
huo, ambayo ni mali ya aliyekuwa askari Polisi, James Kagoma na lingine la
mshtakiwa namba mbili katika kesi hiyo, Elinaza Mshana.
Akitoa hukumu hiyo
iliyochukua muda wa saa Mbili na dakika 30 kuanzia saa 4:20 asubuhi hadi saa
6:30 mchana, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mkoa wa Mbeya, Michael
Mteite, amesema upande wa mashtaka umefanikiwa kuitihibitishia mahakama hiyo
bila shaka kuwa washtakiwa wote watano wametenda kosa hilo Januari 3 mwaka huu,
saa 11 jioni kwenye mlima Kawetele barabara ya kutoka Mbeya kwenda Chunya
kwa kuwapora wafanyabiashara wawili wenye asili ya kiasia shilingi milioni tatu
na nusu na vitu mbalimbali zikiwemo simu mbili za mkononi, laptop mbili na
mabegi matatu ya nguo.
Mbali na askari hao wa zamani, James
Kagoma na Mussa Juma na raia Elinaza Mshana, wengine waliohukumiwa kifungo
hicho ni Mapacha, Mbaruku Hamisi na Amri Kihenya, huku upande wa mashtaka
ukiongozwa na Wakili wa Serikali, Achiles Mulisa akisaidiwa na Basilius
Namkambe na washtakiwa hao wakitetewa na Jopo lililoongozwa na Wakili Ladislaus
Rwekaza akisaidiwa na John Stephen na Daniel Muya.
Hakimu Mteite, amesema mahakama imefikia
uamuzi huo kwa kuzingatia mambo Sita, Kwanza ni kufananana kwa ushahidi wa
uliotolewa na aliyekuwa dereva wa wafanyabiashara hao, Ezekia Matatila na
Mmoja kati wa Wafanyabiashara hao, Pasupuret Sreedhar ambaye ni raia wa India.
Pili ni kuwiana kwa ushahidi wa mashahidi
hao na maelezo ya tukio hilo kutoka kwa Maafisa Wanne wa Polisi waliotoa
ushahidi wao mahakamani hapo ambao ndiyo waliowakamata washtakiwa hao siku ya
tukio.
Tatu ni maelezo ya utetezi ya washtakiwa
hao kuthibitisha kuwa siku ya tukio wote walikuwa pamoja katika eneo la tukio
na muda unaodaiwa kufanyika tukio hilo.
Nne
ni uthibitisho kuwa vitu vyote vinavyodaiwa kuporwa na washtakiwa hao kutoka
kwa Wafanyabiashara hao kukutwa kwenye magari mawili waliyokuwa wakiyatumia
ambayo ni Toyota Cresta namba T 782 BEU mali ya Elinaza Mshana na Grand Mark II
lenye namba za cheses GX 115 6011835 mali ya aliyekuwa askari Polisi,
James Kagoma.
Tano ni jeraha la risasi la
mshtakiwa namba mbili, Elinaza Mshana, kwenye paja lake la mguu wa kulia,
linathibitisha maelezo ya askari polisi kuwa walilazimika kumpiga risasi ya
mguu ili kumzuia asikimbie siku ya tukio hilo.
Na Sita, Hakimu Mteite, amesema kitendo cha Shahidi wa
Kwanza, dereva Ezekia Matatila na Shahidi wa Tatu, Mmoja kati wa Wafanyabiashara
walioporwa, Pasupuret Sreedhar, kuwatambua kwa ufasaha washtakiwa hao
mahakamani hapo.
Kutokana na ushahidi huo, Hakimu Mteite,
amesema mahakama yake imewahukumu washtakiwa hao kifungo cha miaka 30 jela na
kuamuru magari hayo mawili kutaifishwa huku akiondoa adhabu ya kuchapwa viboko
kwa sababu ya huruma kufuatia kupigwa risasi kwa mshtakiwa namba mbili, Elinaza
Mshana.
Hata hivyo, Wakili Kiongozi wa Upande wa
Utetezi, Ladislaus Rwekaza amesema wanataraji kukata rufaa.
Moja ya gari lililotumika katika ujambazi ambalo ni mali ya aliyekuwa askari jemsi |
Post a Comment