Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Ndugu Abbas Kandoro |
Na Mwandishi wetu,Mbeya
MKUU wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro, amesema kitendo cha
Halmashauri ya Mbozi kupata hati yenye mashaka kwa miaka mitatu mfululizo
hakivumiliki, hivyo anafikiria kuzishauri mamlaka zenye uwezo wa kufanya
maamuzi hayo kuivunja Halmashauri hiyo ili kupata mfumo mpya wa kuiendesha.
Hatua hiyo imekuja baada ya ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti wa
hesabu za serikali (CAG) kuonesha kuwa Halmashauri hiyo imepata hati yenye
mashaka, huku kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni 1 zilizopelekwa
na serikali kwa ajili ya shughuli za maendeleo kukosa taarifa sahihi za
kuhifadhi kumbukumbu za mahesabu.
Akizungumza katika kikao maalumu cha baraza la madiwani wa
Halmashauri hiyo, kilichoketi juzi kwa ajenda moja tu ya kupitia mrejesho wa
bajeti ya mwaka wa fedha 2013/14, Kandoro amesema kutokana na kukithiri
kwa vitendo vya ubadhirifu na wizi wa fedha za serikali katika Halmashauri ya
Mbozi, anafikiria kuzishauri mamla zenye uwezo kufanya maamuzi ya
kuivunja Halmashauri hiyo ili kupata mfumo mpya wa kuiendesha.
Awali akitoa salamu za serikali baada ya kikao hicho kufunguliwa,
Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Dk. Michael Kadeghe, alimuomba Mkuu wa Mkoa Kandoro
kuchukua hatua dhidi ya watendaji kwani vitendo vya ubadhirifu ndani ya
Halmashauri hiyo vimekuwa ni vya mazoea.
Kutokana na ombi hilo, Kandoro alikiri kufanyika kwa vitendo hivyo
na kwamba taarifa ya CAG, imeonyesha kuwa kwamba watendaji hao wamezigeuza
fedha za serikali kuwa ni vitega uchumi vyao hivyo ni vema serikali ikachukua
hatua za kisheria.
Amesema, ubadhirifu mkubwa wa fedha umegundulika katika
baadhi ya miradi ya maendeleo hususani kwenye sekta za kilimo, afya,
elimu na maji, ambapo kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni 1 kutokuwa na taarifa
wala kumbukumbu.
Ameyataja baadhi ya maeneo ya miradi ambapo fedha zimeonekana
kutumika ndivyo sivyo au kuibwa kuwa ni shughuli za usafi na uhifadhi wa
mazingira , kiasi cha shilingi milioni 408 zimeonekana kutumika bila maelezo ya
kutosha.
Fedha nyingine kiasi cha shilingi milioni 106,889,500 zilitumika
bila kuwepo na kumbukumbu za msingi kama vile vikao, majina ya wajumbe
hali ambayo iliashiria wazi kuwa kiasi hicho kiliibwa.
Aidha, Kandoro ameendelea kuainisha maeneo mengine kuwa ni Ujenzi
wa maghara katika mji wa Mlowo kiasi cha shilingi milioni 70, ununuzi wa
Pikipiki 92 kukosa stakabadhi za manunuzi.
Ameongeza kuwa, kiasi kingine cha fedha milioni 14 kilionekana
kutumika kwa mashaka katika safari ya watendaji kwenda katika shughuli za
nanenane, milioni 30 zilikosa kabisa maelezo miongoni mwa hoja za mkaguzi.
Kwa mujibu wa maelezo ya watendaji, gunia moja la mahindi hutozwa
ushuru wa kiasi cha shilingi 2000 , hivyo katika gunia hizo 300 Halmashauri
hiyo ilipaswa kupata kiasi cha shilingi 600,000.
Kutokana na hali hiyo, Mkuu wa Mkoa Kandoro, amewataka madiwani
kuwa makini katika kuwasimamia watendaji kwa kuwa wakali dhidi ya wezi na
wabadhirifu kwani huko ndiko kutetea maslahi wananchi waliowachagua.
Hata hivyo, alisikitishwa na taarifa kuwa kuna baadhi ya madiwani
wanatuhumiwa kuwa ni sehemu ya mitandao ya wizi katika Halmashauri hiyo, kwani
hilo linadhihirishwa pale fedha zilizotumwa katika kata zao zimetumika, lakini
kazi hazionekani wala kufanana na gharama.
mwisho
Post a Comment