Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This
Wachezaji wa Taifa Stars wakiwa katika mazoezi yao katika viwanja vya chuo cha uwalimu Msasani mjini Tukuyu Mbeya chini ya Mholanzi Mart Nooij.picha na Keneth Ngelesi

Na EmanuelMadafa
Msafara wa watu 27 wa kikosi cha timu ya Taifa (Taifa Stars) kinaondoka kesho (Julai 30 mwaka huu) saa 10 jioni kwa ndege ya Air Tanzania kwenda Afrika Kusini ambapo kitapiga kambi ya siku mbili kabla ya kuingia Maputo kuikabili Msumbiji (Mambas).

Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager itawasili saa 9 asubuhi kesho (Julai 30 mwaka huu) kwa ndege ya Fastjet kutoka Tukuyu mkoani Mbeya, na baadaye jioni kuunganisha safari ya Afrika Kusini.

Mechi hiyo ya marudiano ya raundi ya pili ya michuano ya Afrika dhidi ya Msumbiji itachezwa Agosti 3 mwaka huu Uwanja wa Taifa uliopo Zimpeto nje kidogo ya Jiji la Maputo.

Msafara huo wa Taifa Stars kwenda Afrika Kusini unajumuisha wachezaji 19 na waliobaki ni maofisa wa Benchi la Ufundi lililo chini ya Kocha Mkuu Mart Nooij kutoka Uholanzi.

Wakati kiungo Mwinyi Kazimoto ametua leo (Julai 29 mwaka huu) nchini kuungana na wenzake, washambuliaji Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu wao wataungana na wenzao kesho (Julai 30 mwaka huu) jijini Johannesburg wakitokea Lubumbashi, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).

Wakati huo huo, Serengeti Boys imewasili salama jana (Julai 28 mwaka huu) jijini Johannesburg kwa ajili ya mechi ya marudiano ya michuano ya Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17 dhidi ya wenyeji Afrika Kusini (Amajimbos).


Serengeti Boys imefikia hoteli ya Garden Court, na mechi hiyo itachezwa Jumamosi (Agosti 2 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Dobsonville uliopo Soweto. Timu hizo zilitoka suluhu katika mechi ya kwanza iliyochezwa karibu wiki mbili zilizopita jijini Dar es Salaam.

Je, Una Habari,Picha,Tangazo,Makala, Ushauri n.k.?Basi Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp 0759 406 070

Post a Comment

 
Top