Watuhumiwa wakifikishwa mahakamani
|
Na EmanuelMadafa,Mbeya
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoani Mbeya,
imewapandisha kizimbani watumishi wawili wa halmashuri ya jiji la
Mbeya, wakiwatuhumu kuomba hongo ya shilingi 150,000 kutoka kwa mwananchi Frank
Mwakaluka.
Watumishi waliofikishwa mahakamani ni Alex Anderson
Kimaro na Julius Issakwisa Mwambulukutu ambapo mshitakiwa namba
moja Alex Kimaro anakabiliwa na mashitaka mawili huku mshitakiwa
namba mbili Julius Mwambulukutu akikabiliwa na shitaka moja.
Akiwasomea mashitaka hayo Mwendedsha Mashitaka wa Takukuru,
Nimroad Mafwele, mbele ya hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama ya Wilaya Girbelt
Ndeuluo, alisema, watuhumiwa hao walitenda kosa hilo November 26,
2013 katika eneo la Ilomba lililopo Jijini Mbeya ikiwa ni kinyume cha sheria
namba 15(i)(a) ya kuzuia na kupambana na rushwa sura ya 11 ya mwaka 2007.
Amesema, kwa nyakati tofauti watumishi hao wakiwa
katika ukaguzi wa majengo walimkamata Franky Mwakaluka kwa madai ya
kushindwa kulipia jengo lake na kumuomba kiasi cha shilingi 150,000 ili
wamuachie na kwamba zoezi hilo lilifanyika ndani ya gari ambalo
ni mali ya halmashauri ya Jiji la Mbeya.
Aidha, Mwendesha mashitaka huyo, amemsomea shitaka la pili
mshitakiwa namba moja ambaye ni Alex Kimaro.
Alisema mshitakiwa huyo akiwa katika ukaguzi wa majengo aliomba
hongo ya shilingi 60,000 kwa Green Mwakionya ili amuachie huru Franky Mwakaluka
waliyekuwa wamemkamata kwa madai ya kutolipia kodi ya pango.
Baada ya watuhumiwa hao kusomewa makosa mbalimbali, mwanasheria
huyo alisema dhamana ipo wazi na masharti ya dhamana lazima yazingatiwe kwa
mujibu wa vifungu vya sheria vya kosa vinavyoeleza.
Hata hivyo, baada ya mwanasheria huyo kuwasilisha maombi hayo,
hakimu Ndeuruo, alisema dhamana ipo wazi kwa washitakiwa wote wawili
na kwamba kila mshitakiwa atatakiwa kudhaminiwa na mtu mmoja kwa
kiasi cha shilingi milioni moja na kwamba kesi hiyo itasikilizwa tena Oktoba 13
mwaka huu.
Washitakiwa wote walikana mashitaka na kwamba wapo nje
kwa dhamana baada ya kufanikiwa kudhaminiwa.
Post a Comment