Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF) limewapeleka wanamichezo 12 wakiwemo viongozi, makocha na wachezaji kwenye
Kamati ya Nidhamu kwa ajili ya kuchukuliwa hatua za kinidhamu kutokana na
matukio mbalimbali kwenye Ligi Daraja la Kwanza (FDL) na michuano ya Kombe la
Taifa la Wanawake.
Wachezaji Dihe Makonga, Swalehe Idd
Hussein, Ramadhan Mwinyimbegu na Shaibu Nayopa wa Oljoro JKT, na Nassib Lugusha
wa Polisi Dodoma wanalalmikiwa katika Kamati ya Nidhamu kwa kushambulia waamuzi
na kufanya vurugu kwenye benchi la timu pinzani katika mechi zao za FDL.
Mtunza Vifaa (Kit Manager) wa Polisi
Mara, Clement Kajeri analalamikiwa kwa kuongoza mashambulizi dhidi ya waamuzi
kwenye mechi kati ya timu yake na Mwadui iliyochezwa Uwanja wa Kumbukumbu ya
Karume mjini Musoma.
Naye Mtunza Vifaa (Kit Manager) wa Rhino
Rangers, Albert Mbunji anapelekwa katika Kamati hiyo kwa kupinga maamuzi na
kuwatukana waamuzi kwenye mechi dhidi ya Polisi Dodoma iliyochezwa Uwanja wa
Jamhuri mjini Dodoma.
Pia Mtunza Vifaa (Kit Manager) wa Oljoro
JKT, Eliud Justine Mjarifu analalamikiwa kwa matukio mawili; alimpiga Kocha wa
Burkina Faso, CR Mwakambaya kwenye mechi ya FDL iliyochezwa Uwanja wa Jamhuri
mjini Morogoro. Pia alimtukana mwamuzi akiba (fouth official) Mussa Magogo
kwenye mechi dhidi ya Toto Africans iliyochezwa Uwanja wa CCM Kirumba jijini
Mwanza.
Kocha wa Polisi Tabora, Kim Christopher
analalamikiwa kwa kumtolea mlugha chafu mwamuzi wa mechi kati ya timu yake na
Panone FC iliyochezwa Uwanja wa Ushirika mjini Moshi.
Msimamizi wa Kituo cha Musoma, Katibu wa
Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mara (FAM), Mugisha Galibona naye anapelekwa
katika Kamati ya Nidhamu kwa tuhuma za kutotoa ushirikiano kwa maofisa wa mechi
na kuchochea maofisa hao (waamuzi) kupigwa.
Kwa upande wake, Kamati ya Mpira wa
Miguu wa Wanawake ya TFF imependekeza Katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa
wa Simiyu, Emmanuel Sologo, na Kaimu Katibu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa
Singida (SIREFA), Gabriel Gunda kupelekwa kwenye kamati ya Nidhamu kwa matukio
mbalimbali yaliyojitokeza kwenye mechi za Kombe la Taifa la Wanawake.
Sologo anatuhumiwa kumpiga kibao mwamuzi
wa mechi ya marudiano kati ya timu yake ya Simiyu na Shinyanga iliyochezwa
mjini Shinyanga, tukio ambalo lilimfanya mwamuzi huyo avunje mchezo.
Naye Gunda analalamikiwa kwa kushindwa
kuhakikisha timu yake ya Singida inaingia uwanjani kwenye mechi ya marudiano
dhidi ya Dodoma iliyokuwa ifanyike kwenye Uwanja wa Namfua mjini Singida.
MWISHO
Post a Comment