Madalali wa mahakama Kampuni ya Jagro enterprises limited wakiendelea na shughuli za ufungaji wa kitio hicho cha Mek One kilichopo Tukuyu Mbeya. |
Na Emanuel Madafa,Mbeya.
MAHAKAMA Kuu leo, imekifunga kituo cha mafuta ya Petrol na Dizeli
cha Mek One kilichopo Wilayani Rungwe, baada ya kukiuka amri ya mahakama hiyo
iliyokitaka kituo hicho kusitisha huduma mpaka kesi ya msingi namba 6/2013 iliyopo katika mahakama
ya Wilaya ya Rungwe itakapotolewa maamuzi.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Msajili wa
mahakama Aron Lyamuya, amesema, kituo hicho ambacho kinamilikiwa na Halmashauri
ya Wilaya ya Rungwe, kiliingia mgogoro na Kampuni ya mafuta ya GAPCO na kuvunja mkataba hali iliyomfanya mmiliki huyo
kufungua kesi katika mahakama ya Wilaya ya Rungwe
Amesema, wakati kesi hiyo inaendelea halmashauri hiyo imeingia mkataba mpya na Kampuni ya mafuta
ya Mek One, jambo lililomsukuma mmiliki wa awali ambaye ni GAPCO kufikisha
barua ya malalamiko kwenye mahakama kuu.
Amesema, Oktoba 8, 2013, mahakama kupitia hukumu iliyotolewa na
Jaji Atuganile Ngwala, iliitaka halmashauri ya Rungwe, kutofanya jambo lolote katika kituo hicho, lakini
inaonekana amekaidi amri hiyo hivyo, mahakama imempa dahama Kampuni ya JAGRO kukifunga kituo hicho.
Aidha, amesema kuwa sambamba na kukifunga kituo hicho pia,
mahakama hiyo inatarajia kuwafungulia kesi, mkurugenzi wa halmashauri ya Rungwe
Veronica Kessy na mkurugenzi wa Kampuni ya Mek One Mohamed Awadhi kwa kosa la
kukiuka amri ya mahakama.
Hata hivyo, akikifunga kituo hicho cha mafuta, Mkurugenzi wa
Kampuni ya Jagro inayoshughulika na masuala ya udalali Mkoa wa Mbeya,Maulid
Hamis ,amesema wao wanatekeleza agizo la mahakama, ambalo limewapa dhamana ya
kukifunga kituo hicho, pia ni moja ya majukumu yanayofanywa na kampuni hiyo.
Mwisho.
Post a Comment