Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ikiendelea na ziara katika eneo la kituo cha kupooza na kusambaza umeme kilichopo Njiro nje kidogo ya jiji la Arusha. |
Wataalam kutoka kampuni ya Sweco International AB, wakiendelea na ujenzi katika kituo cha kupooza na kusambaza umeme cha Njiro kilichopo nje kidogo ya jiji la Arusha. |
Na Greyson Mwase, Arusha
Meneja
Mradi wa Kusambaza Umeme unaojulikana kwa jina la Electricity V
unaofadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Mhandisi Florence
Gwang’ombe amesema kuwa tatizo la kukatika katika kwa umeme katika
mkoa wa Arusha litakwisha mapema Juni mara baada ya kukamilika kwa
kituo cha kupooza na kusambaza umeme kilichopo katika eneo la Njiro,
nje kidogo ya jiji la Arusha.
Mhandisi
Gwang’ombe aliyasema hayo mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Nishati na Madini iliyofanya ziara katika kituo hicho ili kujionea
maendeleo yake pamoja na kuishauri serikali jinsi ya usimamizi wake.
Alisema
mara baada ya kukamilika kwa ujenzi wa kituo hicho mbali na kuboresha
upatikanaji wa nishati ya umeme katika jiji la Arusha, wateja wapya
wapatao 30,000 wanategemewa kuunganishiwa umeme kutoka katika kituo
hicho.
Akielezea
mradi huo kwa ujumla Mhandisi Gwang’ombe alisema kuwa mradi huo
unaofadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa mkopo wa
kiasi cha shilingi za kitanzania 72,588, 506,400 unahusisha ujenzi wa
njia za umeme wenye urefu wa kilomita 480 za msongo wa kilovoti 33 na
ufungaji wa transfoma 102 za kusambaza umeme zenye ukubwa wa 33/0.4 kV.
Alisema
pia mradi huu unahusisha ujenzi na ukarabati wa vituo vya kupoozea
umeme vya Ilala, Sokoine katika mkoa wa Dar es Salaam na upanuzi wa
kituo cha kupoozea umeme cha Njiro.
Alisisitiza
kuwa mradi unatekelezwa na Mkandarasi National Contracting Company
ambaye alishinda zabuni ya ujenzi na ukarabati wa vituo vya kupoozea
umeme katika mikoa ya Dar es Salaam na Arusha na mkandarasi Eltel
Networks TE AB ambaye alishinda zabuni ya ujenzi na ukarabati wa mifumo
ya kusambazia umeme katika mikoa ya Shinyanga na Mwanza.
Akielezea
hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa kituo cha kupoozea umeme cha Njiro,
Mhandisi Gwang’ombe alisema kazi zinazoendelea katika kituo hicho ni
pamoja na ufungaji wa transfoma mbili na ufungaji wa mitambo ya kisasa
kwa ajili ya kuendesha na kulinda mifumo ya umeme.
Aliongeza
kuwa uagizaji na utengenezaji wa vifaa umekamilika kwa asilimia 85,
kazi za ujenzi zimekamilika kwa asilimia 76 pamoja na kumalizika kwa
kufunga na kuunganisha vifaa na mifumo ya umeme.
Alisisitiza
kuwa mradi huu unategemewa kuongeza ukuaji wa uchumi katika mkoa wa
Arusha pamoja na mikoa mingine kama Shinyanga na Mwanza kwani
utachochea ukuaji wa viwanda vidogo vidogo na biashara katika maeneo
husika pamoja na kuongeza fursa za ajilra kwa wananchi.
Aliendelea
kusema kuwa mradi huo utaboresha huduma za jamii kwa wananchi kutokana
na upatikanaji wa umeme mashuleni, mahospitalini na kwenye maeneo
mengine ya jamii husika na hivyo kupunguza umasikini kwa wananchi
jambo ambalo linaendana na malengo ya siasa ya nchi.
Akizungumzia
lengo la mradi, Mhandisi Gwang’ombe alisema kuwa lengo la mradi ni
kuongeza uwezo wa kusambaza umeme wenye kiwango kinachotakiwa na
usiokatikakatika na kulisaidia Shirika la Umeme Nchini (Tanesco)
kuweza kuwafikia na kuwapatia umeme wenye uhakika wateja wengi zaidi
ambao bado hawajapatiwa huduma ya umeme.
Wakati
huo huo, Mkurugenzi wa Shirika la Umeme Nchini (Tanesco), Mhandisi
Felchesmi Mramba aliiambia Kamati ya Bunge kuwa ongezeko la wateja wa
kawaida na viwanda lilisababisha ongezeko la kasi la matumizi kufikia
Megawati 70 hali iliyopelekea shirika kuboresha na kujenga vituo
vya kupoozea na kusambazia umeme.
Mhandisi
Mramba alisema, kabla ya ujenzi wa kituo hicho, hali ya umeme katika
jiji la Arusha ilikuwa ni mbaya hali iliyopelekea ujenzi wa kituo hicho
na kusisitiza kuwa Shirika limeamua kufanya mapinduzi katika sekta ya
umeme kwa kuhakikisha linashirikiana na wawekezaji mbalimbali na
wataalamu wake katika ujenzi wa vituo vya kuzalisha na kusambaza umeme
ili kuzalisha nishati ya umeme ya uhakika.CREDIT MICHUZI MATUKIO
Post a Comment