Timu
ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) imepoteza mchezo wake wa kwanza wa
michuano ya COSAFA Castel Cup dhidi ya timu ya Taifa ya Swaziland, baada
ya kufungwa bao 1- 0 mchezo uliochezwa katika uwanja wa Royal Bafokeng
jijini Rustenburg.
Stars
ilipoteza nafasi zaidi ya tano kipindi cha kwanza kupitia kwa
washambuliaji wake Saimon Msuva na nahodha John Bocco ambao walishindwa
kukwamisha mpira wavuni katika kipindi cha kwanza, ambacho Taifa Stars
ilicheza vizuri.
Swaziland
walipata bao lao la kwanza na la ushindi dakika ya 42 ya mchezo, kupitia
kwa mlinzi wa kulia Sifiso Mabila aliyepanda kuongeza nguvu ya
mashambulizi na kuachia shuti lililouacha mlinda mlango wa Stars akikosa
cha kufanya kuokoa mchomo huo.
Kipindi cha
pili Stars walizidiwa kwani mashambulizi yao hayakua na madhara langoni
mwa Swaziland na kumuacha mlinda mlango Mphikeleli Dlamnini akiwa likizo
kwa muda mrefu.
Mara
baada ya mchezo kocha wa Stars Mart Nooij alisema, amepoteza mchezo wa
kwanza ambao alitegemea kupata ushindi, vijana walicheza vizuri kipindi
cha kwanza, lakini bao la mapema lilionekana kuwapoteza mchezoni.
“Presha ya
mchezo ilikua kubwa hasa kipindi cha pili, kutokana na vijana wangu
kucheza kwa kusaka bao, huku Swaziland wakimiliki zaidi mpira na kukuta
mipango yetu kutokua na madhara” alisema Nooi.
Akiongelea
michuano ya COSAFA amesema anashukuru kwa kupata mwaliko huu, kwani
kwake anatumia michuano hii kama sehemu ya maandalizi ya kuwania kufuzu
kwa fainali za mataifa Afrika (AFCON, CHAN) mwezi juni, huku akisema
anaamini wachezaji aliowacha majeruhi nyumbani pamoja na wachezaji wa
kimataifa wanaochezea klabu ya TP Mazembe, wataongeza nguvu katika
kikosi chake watakaporejea Tanzania.
Baadhi
ya watanzania waishio nchini Afrika Kusini walijitokeza uwanja wa Royal
Bafokeng kuishangilia timu ya Taifa ya tanznaia Taifa Stars wakiwa
sambamba na maofisa wa ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini.
Taifa
Stars itacheza mchezo wake wa pili siku ya jumatano saa 11 za jioni kwa
saa za Afrika kusini, sawa na saa 12 jioni kwa saa za Afrika Mashariki
dhidi ya Madagascar katika uwanja wa Royal Bafokeng., ambao katika
mchezo wa awali wamibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Lesotho.
Wakati
huo huo kiungo wa Taifa Sars Said Juma “Makapu” ambaye anasumbuliwa na
majeruhi, anatarajiwa kurejea nyumbani Tanzania leo kwa ajili ya kupata
vipimo zaidi na matibabu.






Post a Comment