Makamu
wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad,
akiwamuwakilisha Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein, katika
ufunguzi wa mkutano wa Kimataifa wa muziki kwa nchi za jahazi,
inaofanyika chuo cha muziki Forodhani Zanzibar.
Mkurugenzi wa Chuo cha Muziki Zanzibar bibi Fatma Kilua, akimkaribisha mgeni rasmi Maalim Seif katika ufunguzi za mkutano huo.CREDIT MICHUZI -MATUKIO
Muandaaji wa mkutano huo Profesa Raymond Vogals, akizungumza machache kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi.
Baadhi
ya washiriki wa mkutano huo wa kimataifa wa muziki, wakisikiliza hotuba
ya mgeni rasmi Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad kwa niaba ya Dkt. Shein.
Mwanafunzi wa Diploma katika chuo cha muziki Zanzibar Gora Mohamed (kulia), akitumbuiza katika hafla ya ufunguzi wa mkutano huo.
Makamu
wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad,
akisalimiana na baadhi ya washiriki wa mkutano huo wa muziki, baada ya
kuufungua rasmi huko chuo cha muziki Forodhani Zanzibar.
Makamu
wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akiwa
katika picha ya pamoja na baadhi ya washiriki wa mkutano wa kimataifa wa
muziki unaofanyika chuo cha muziki Forodhani Zanzibar. (Picha na Salmin
Said, OMKR)
Na: Hassan Hamad (OMKR)
Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein,
amesema sanaa ya muziki ina nafasi kubwa ya kuendeleza amani na
maelewano duniani.
Amesema
kupitia sanaa hiyo wanamuziki kutoka pembe tofauti za dunia wamekuwa
wakikutana kubadilishana uzoefu na kusoma tamaduni za kila upande, jambo
ambalo husaidia pia kuzitangaza nchi na tamaduni zao katika ramani ya
dunia.
Dkt.
Shein ameeleza hayo huko chuo cha muziki Forodhani, katika hotuba yake
iliyosomwa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif
Sharif Hamad, wakati akifungua mkutano wa kimataifa wa siku nne wa
muziki kwa nchi za jahazi.
Amesema
Zanzibar ikiwa nchi yenye historia ya muziki hasa wa Taarab, imekuwa
ikijifunza kutoka kwa wanamuziki wa nchi nyingi duniani zikiwemo India,
Misri na nchi za Afrika kama vile Nigeria, Congo na Comoro, jambo ambalo
limeifanya Zanzibar kuwa na uhusiano wa karibu wa kiutamaduni na nchi
hizo.
Amefahamisha
kuwa Zanzibar inakusudia kuibua na kuendeleza vipaji vya wanamuziki
wachanga, na kwamba mkutano huo utatoa fursa kwa wanamuziki wa Zanzibar
kujifunza mbinu mbali mbali za muziki zitakazosaidia kukuza vipaji vyao.
Katika
hotuba hiyo Dkt. Shein amewataka washiriki wa mkutano huo kuijadili kwa
uwazi maudhui ya mkutano huo, ili kufikia malengo ya kukuza muziki wa
Afrika ambao ni muhimu katika kukuza maelewano miongoni mwa nchi na
wananchi wa mataifa hayo kwa ujumla.
Ameeleza
kuwa Zanzibar inajivunia historia ya muziki wa taarab asilia iliyopata
umaarufu mkubwa kutokana na mwimbaji wake wa mwanzo marehemu Siti Bin
Saad kuanzia miaka ya 1920’s, hatua ambayo imepelekea kuibuka kwa muziki
wa kisasa wa taarab “modern taarab”, ambayo imekuwa ikipendwa na vijana
wengi wa ndani na nje ya nchi.
Naye
Mkurugenzi wa Chuo cha Muziki Zanzibar bibi Fatma Kilua, amesema
kufanyika kwa mkutano huo hapa Zanzibar ni fursa pekee kwa wanamuziki wa
Zanzibar kujifunza na kuitangaza katika fani hiyo.
“Kama
chuo tumefarijika sana kuwa mwenyeji wa mkutano huu wa kimataifa ambao
utatoa fursa kwa vijana wetu kujifunza mbinu mbali za muziki”, alieleza
bi. Kilua.
Kwa
upande wake muandaaji wa mkutano huo Profesa Raymond Vogals amesema,
sanaa ya muziki imekuwa ikipata maendeleo makubwa duniani, na tayari
wanamuziki kadhaa wameshahitimu shahada ya uzamivu (PHD) katika fani
hiyo wakiwemo pia kutoka bara la Afrika.
“Muziki
ni taaluma ambayo imekuwa ikipata mafanikio makubwa duniani, kwa hivyo
tusome muziki wa Kiafrika ili kuendeleza taalum hii ambayo pia husaidia
kutoa ajira”, alisisitiza Prof. Raymond.






Post a Comment