Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This
Mheshimiwa January Makamba akisalimiana na baadhi ya watoto wenye ulemavu wa ngozi Albino mara baada ya kutembelea kituo cha kulelea watu wenye tatizo hilo Buhangija Shinyanga.Picha Tanzania Mpya

Miezi karibu miwili iliyopita, rafiki zangu wawili, Masoud Kipanya na Henry Mdimu, ambao wako mstari wa mbele kupinga unyanyasaji na mauaji ya watu wenye Albinism, walinijulisha kuhusu kituo cha Buhangija, kinachohifadhi watoto wenye Albinism, watoto yatima na wenye ulemavu wa kusikia kilichoko Shinyanga. Kituo hiki kina watoto takriban 400. Wazazi wa watoto hawa wamewaleta na kuwaacha hapa kituoni kwasababu huko vijijini watoto wao wanawindwa na wauwaji wenye imani za kichawi.
Juzi, mimi na mke wangu tulifika Mwanza kutafuta wadhamini kwenye mchakato wetu wa uchaguzi ndani ya CCM. Nilifanya mazungumzo na wadau kadhaa wa harakati za kupinga mauaji ya albino. Nao pia wakataja Buhangija. Kwahiyo, tulipokwenda Shinyanga na basi letu jana, baada ya shughuli ya kupata udhamini kuisha, tukaona tutumie fursa ya kuwa tuko Shinyanga walau hata nusu saa kutembelea kituo cha Buhangija. Tuliishia kukaa masaa matatu. Tuliguswa na mazingira na changamoto za kituo kile. Tuliguswa zaidi na upendo wa watoto wale kwa kuwa saa zote walipenda kubebwa na kushikwa na kukumbatiwa. Haikuwa rahisi kwetu kuondoka haraka.
Kituo kile kinahitaji msaada mkubwa. Kuna shida ya kila kitu: mabweni, vitanda, magodoro, shuka, vyandarua, mashuka, madawa - kila kitu. Lakini shida kubwa zaidi ni vyakula. Mlo mmoja pale ni kilo 70 za unga/mchele, kilo 70 za maharage, bado mafuta, sukari na maji. Mkaa unaotumika kwa siku ni gunia moja na nusu.
Mtoto mdogo kuliko wote pale ana miezi 18 na mkubwa zaidi ana miaka 24. Ukiongea nao, wana ndoto kubwa za maisha yao. Lakini pia wanajua kwamba maisha yao yapo hatarini na wale wadogo zaidi wanapata shida kuelewa ni kwanini.
Wapo wafadhili kadhaa ambao wamekuwa wanakisaidia kituo. Baadhi ya taasisi zimeajiri walimu na walezi wa ziada. Wamefanya kazi nzuri, kazi ya Mungu. Wanastahili pongezi na shukrani. Mimi na mke wangu tumetoa msaada wa mahitaji yote ya wiki mbili. Lakini wiki mbili zitaisha. Bado misaada inahitajika. Cha msingi ni utaratibu endelevu (sustainability) ya kupata rasilimali za kuendesha kituo. Nimezungumza na walimu kuhusu namna endelevu na ya uhakika ya kuendesha kituo. Kuna mawazo kadhaa ya kufanyiwa kazi. Lakini kwasasa, kama utapenda kusaidia, tafadhali wasiliana na Mwalimu Peter Ajari kwa namba 0757 611 930. Lakini zaidi ukipita Shinyanga, hata kama huna cha kutoa, usiache kutembelea Buhangija kwasababu watoto hawa wanahitaji pia upendo, kwani wengi wao wazazi wao walivyowaacha hawajarudi tena. ‪#‎TanzaniaMpya‬





Je, Una Habari,Picha,Tangazo,Makala, Ushauri n.k.?Basi Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp 0759 406 070

Post a Comment

 
Top