Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This
Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akizungumza na viongozi wa CUF pamoja na wagombea uwakilishi na ubunge wa Chama hicho Wilaya za Unguja katika ukumbi wa majid Kiembe Samaki.
Viongozi wa CUF pamoja na wagombea uwakilishi na ubunge  wakimsikiliza Katibu Mkuu wa Chama hicho Maalim Seif Sharif Hamad wakati akihutubia kwenye ukumbi wa Majid Kiembesamaki.
Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar Ismail Jussa Ladhu, akinukuu baadhi ya vifungu vya katiba ya chama hicho vilivyoipa uhalali  Kamati tendaji ya chama hicho Taifa kufanya uteuzi ya wagombea katika majimbo yaliyoongezwa kulingana na hali halisi ilivyokuwa.

Katibu Mkuu wa CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad akikabidhi vifaa vya michezo kwa viongozi wa wilaya na wagombea wa majimbo kama vitendea kazi vya kampeni, ambapo kila jimbo lilikabidhiwa seti 40 za jezi na mipira 120.
Na Khamis Haji, (OMKR)
 
Katibu Mkuu wa Chama cha Wanancfhi CUF, Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad amesema upepo wa kisiasa Zanzibar unakivumia vyema chama hicho na matarajio ni kupata ushindi wa kishindo ambao haujawahi kutokea wa asilimia 80 katika uchaguzi mkuu wa mwezi Oktoba.

Maalim Seif amesema hayo jana alipokuwa akiwahutubia viongozi wa Wilaya na majimbo wa chama hicho huko Kiembesamaki, ambapo pia alitangaza timu itakayo kiongoza chama hicho kupata ushindi katika uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba 25.
Maalim Seif amesema kwa namna wananchi wanavyokikubali chama hicho na namna kilivyojipanga na iwapo kila kiongozi na mwanachama atatekeleza majukumu yake bila ya kulalamika kitachukua idadi kubwa ya majimbo ya uchaguzi na kushinda nafasi ya Urais kwa kishindo.
“Mazingira yaliyopo Zanzibar ni mazuri sana kwa CUF kupata ushindi ambao haujawahi kutokea, hivyo kila mmoja wetu aongozwe na dhamira ya kuchukua nchi mwaka huu, na mara hii haibiwi mtu kura yoyote”, alisema Maalim Seif.  
Alisema malengo ya CUF katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu ni kuwa na idadi ya kutosha ya majimbo yatakayo kiwezesha kufanikisha kikamilifu mipango yake ya kuwaletea matumaini na maisha bora Wazanzibari chini ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Katika mkutano huo ambao umehudhuriwa na wagombea waliopitishwa na chama kwa upande wa Unguja, Maalim Seif amemtangaza Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui kuwa ndiye Meneja wa Kampeni za Urais wa Zanzibar, akisaidiwa na mshauri wake wa Mikakati, Mansour Yussuf Himid.
Aidha kwa upande wa Pemba, Maalim Seif alisema Mratibu wa kampeni hizo ni Mjumbe wa Baraza Kuu la Uongozi, Hamad Masoud Hamad akisaidiwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, Said Ali Mbarouk.
Maalim Seif alisema Zanzibar hakuna hata jimbo moja ambalo chama hicho kinaweza kusema kwamba hakina matumaini ya kushinda na kwamba suala la kushinda au kutoshinda litategemea chama hicho kimejipanga vipi kuchukua ushindi.
Katibu Mkuu huyo wa CUF ameonya kuwa huu si wakati wa viongozi na wanachama kuvutana na wala si wakati wa kukumbatia ubinafsi kwa baadhi yao kupeana majukumu wasiyo yamudu kwa kwa kuzingatia urafiki au ujamaa.
Kaimu Naibu Katibu Mkuu, Ismail Jussa Ladhu alisema CUF katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu CUF kitakuwa na kampeni ya aina yake kwa makusudi ya kuwathibitishia Wazanzibari na nchi nzima kuwa kweli kimejiandaa kuiongoza Zanzibar.
Jussa alisema Agosti 22 wagombea wote waliopitishwa na chama kugombea Uwakilishi watakwenda kuchukua fomu Tume ya Uchaguzi Zanzibar kwa sherehe kubwa ili kila mtu apate habari kuwa safari ya chama hicho kuiongoza Zanzibar na kutimiza matarajio yao i imezna rasmi.
“Siku hiyo wagombea wote wa Uwakilishi Zanzibar watakwenda kuchukua fomu, mwenye kupiga dufu, mwenye kupiga mbwa kachoka, mwenye kupiga rusha roho ni ruhusa kufanya sherehe hizo”, alisema Jussa.
Kaimu Naibu Katibu Mkuu huyo alisema kwa upande wa nafasi ya Urais wa Zanzibar, ambayo mgombea wake ni Maalim Seif Sharif Hamad atakwenda kuchukua fomu ya kuwania nafasi hiyo Agosti 23, ambapo pia chama hicho kimeandaa shamra shamra za aina yake.  
Katika mkutano huo, Maalim Seif aliwakabidhi viongozi wa Wilaya na majimbo seti 40 za jezi kwa kila jimbo moja pamoja na mipira 120. 

Je, Una Habari,Picha,Tangazo,Makala, Ushauri n.k.?Basi Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp 0759 406 070

Post a Comment

 
Top