Kiongozi wa shirikisho la soka
barani Afrika Issa Hayatou kutoka Cameroon amepewa jukumu la kuongoza
shirikisho la soka duniani Fifa kwa muda.
Hayatou atachukua
usukani kufuatia kusimamishwa kazi kwa Rais wa Fifa Sepp Blatter kwa
muda wa siku 90 na Kamati ya Maadili ya shirikisho hilo, shirikisho hilo
linalosimamia soka duniani limesema kupitia taarifa.
Hayatou,
aliyeongoza CAF tangu 1988, atachukua usukani kwa mujibu wa sheria za
Fifa, akiwa ndiye makamu wa rais katika kamati tendaji ya Fifa
aliyehudumu muda mrefu zaidi.
Baadaye, Hayatou ametoa taarifa na kusema amepokea majukumu hayo mapya lakini ataongoza tu kwa muda.
“Rais mpya atachaguliwa kwenye Mkutano Mkuu Februari 26, 2016. Na mimi mwenyewe sitawania,” amesema kupitia taarifa.
“Hadi
mkutano huo ufanyike, naahidi kwamba nitajitolea kwa nguvu zangu zote
kutumikia shirikisho hili, mashirikisho wanachama, waajiri wetu,
washirika na mashabiki wa soka popote walipo.”
Aidha, ameahidi
kuendelea kushirikiana na watawala na kuendeleza uchunguzi kwenye
shirikisho hilo lililoyumbishwa na madai ya ulaji rushwa.CHANZO BBC
Post a Comment