Mahakama Kuu nchini Rwanda imemhukumu kifungo cha maisha jela mhubiri aliyehusika katika mauaji ya kimbari ya 1994.
Jean Uwinkindi alipatikana na hatia ya kupanga na kushiriki katika mashambulio dhidi ya Watutsi, mahakama ilisema.
Mchungaji huyo wa umri wa miaka 64, kutoka jamii ya Wahutu, ndiye mshukiwa wa kwanza wa mauaji ya kimbari kutumwa Rwanda akajibu mashtaka na iliyokuwa mahakama maalum ya UN iliyoendesha shughuli zake kutoka Arusha, Tanzania.
Mahakama hiyo ilifungwa mwezi jana baada ya kuwapata na hatia watu 61 na kuwaachilia wengine 14.
Uwinkindi, aliyekuwa kiongozi wa kanisa la kipentekoste viungani mwa mji mkuu Kigali, alikuwa amepinga kurejeshwa kwake Rwanda.
Alisema hangepata hati Rwanda, ambayo sasa inaongozwa na Watutsi.
Mawakili wake wamesema atakata rufaa uamuzi huo wa mahakama huu.
“Mahakama imebaini kwamba kulitokea mauaji ya Watutsi katika milima ya Rwankeri and Kanzenze na mashambulio hayo yaliongozwa na Uwinkindi," alisema Jaji Kanyegeri Timothee, kama alivyonukuliwa na shirika la habari la Reuters.
Upande wa mashtaka uliambia mahakama kwamba uchunguzi uliofanywa baada ya mauaji hayo uligundua miili 2,000 karibu na kanisa hilo la Kanzenze.
Uwinkindi alifunguliwa mashtaka 2011 baada ya kukamatwa 2010 katika nchi jirani ya Uganda.
Mshukiwa mwingine mkuu, Ladislas Ntaganzwa, alikamatwa wiki mbili zilizopita nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.chanzo bbc
Post a Comment