Na
Krantz Mwantepele .Kahama
Wanawake ni nguzo
muhimu sana katika uchumi wa watanzania wengi. Mwanamke ana ushawishi mkubwa na
hasa pale anapoamua kuwa chachu ya maendeleo. Na hasa anapowezeshwa kufanya
hivyo.
Katika
kufanikisha hili waraghbishi wameamua kutoa mafunzo ya uraghbishi kwa makundi
mengine ya jamii. Mojawapo ya kundi hilo ni la wanawake. Waraghbishi wapya toka
katika kijiji cha Nyandekwa, kati ya hao wapo 9 ambao ni wanawake.
Mmoja
wao ni Anna Alphonce, Mwenyekiti wa kitongoji cha Busolo, katika kijiji cha
Nyandekwa. Akielezea jinsi alivyoanza uraghbishi alisema:
“Mi
niliona kuna kikundi wanakaaga humu karibu kila jioni. Na kila nilipokuwa
napita jirani na hapa naona watu wamejaa, basi nikapenda namimi nijiunge nao na
hasa baada ya kujua nini wanafanya. Na hapo ndipo nilipoanza uraghbishi,”
Anna Alphonce
(katikati) ambaye ni Mwenyekiti wa Kitongoji cha Busolo akifafanua jambo wakati
akielezea uraghbishi anaofanya .
Akiwa
kama mwenyekiti mwanamke wa kitongoji aliweza kutumia nafasi yake kufanya
uraghbishi kwa anaowaongoza. Kwa kuwa kilikuwa ni kipindi cha kampeni za
uchaguzi mkuu, aliitisha mikutano kwenye kitongoji chake kwa lengo la kutoa
hamasa ya wananchi kujitokeza kwa wingi. Kwa nafasi yake aliweza kuyafikia
makundi ya wazee, vijana na wanawake. Ingawa kati ya hawa wanawake ndio
walikuwa washiriki wazuri.
“Msisitizo
kwenye mikutano yangu ilikuwa ni kupiga kura kwa amani. Niliwasihi Vijana wetu
wasiwe chanzo cha vurugu na badala yake wawe walinzi na kuhakikisha uchaguzi
unafanyika katika mazingira ya utulivu,”
Haya
ni maelezo ya mwenyekiti huyo akielezea jinsi alivyotumia nafasi yake kwenye
kufanya hamasa ya amani. Akaongeza,
“Kwangu
mimi haya ni mafanikio kwa sababu kweli uchaguzi umefanyika kwa amani katika
kitongoji change.”
Mraghabishi
mwingine ni Matrida Peter toka katika kijiji cha Nyandekwa, yeye uraghbishi
wake alifundishwa na Elizabeth Ngaljalina toka kijiji hicho hicho. Baada ya
kufundishwa yeye alichoamua kufanya uraghbishi kwa vijana wa kijiji cha
Nyandekwa pamoja na wale waliokuwa mashuleni pia.
Akielezea
jinsi ambavyo anafanya uraghbishi kwa vijana, Matrida anasema,
“Nafundisha
makuzi ya ujana ili kuweza kutimiza ndoto zao. Kwanza nawaelewesha kuhusu
mabadiliko ya miili yao hasa wanapoingia hatua ya kubalehe na kuvunja ungo. Hii
inawasaidia jinsi ya kujikinga na maambuzi ya virusi vya ukimwi.”
Uraghbishi
wake hauishii kwa vijana walio nje ya shule, hivyo alikwenda kumtembelea ili
aweze kupata fursa ya kutoa elimu hiyo hasa kwa wanafunzi ya shule ya msingi.
Walengwa wakubwa wakiwa ni wanafunzi wa kuanzia darasa la nne mpaka la saba.
Akielezea rika la watoto hao, Matrida anasema:
“Watoto
wa siku hizi wana maumbo makubwa, hivyo hao wa darasa la nne mpaka la saba sio
wadogo kiumbo na wengi ndio wapo kwenye huo umri. Wanahitaji mwongozo manake
makuzi siku hizi yameachwa kwa wazazi na wao mda mwingine wanaona aibu kuongea
nao,”
Matokeo
ya uraghbishi huu wa mwanamama Matrida ni kuongeza kwa watoto wenye uelewa wa
mipango ya uzazi na maambukizi ya virusi vya Ukimwi. Kwani maambukizi katika
wilaya ya Kahama yapo juu kutokana na shughuli za uchimbaji wa madini.
Uraghbishi
una maana tofauti tofauti kwa wanawake hawa wa kijiji cha Nyandekwa, kama
anavyoelezea Mariam Stephano aliyeanza uraghbishi mwezi Septemba 2015:
“Uraghbishi
kwangu mimi ni kutetea haki za vijana na mabinti, na sio tu kutetea bali kujua
na falsafa yake ya jinsi ya kutenda ili kufanikisha lengo hilo ninaloliangalia
kama ndio jukumu langu,”
Wakati
Suzan Stephano yeye analinganisha uraghbishi na haki za kikatiba. Huku
akisisitiza umuhimu wa kuthaminiwa kwa mwanamke katika kijiji chao na taifa kwa
ujumla. Na yeye pia anakiri kwa uraghbishi ni falsafa ya jinsi ya kutenda.
Waraghbishi
wanawake toka katika kijiji cha Nyandekwa wakimsikiliza Mwenyekiti wa Kitongoji
cha Busola akielezea uraghbishi wake katika ngazi ya kitongoji
Mraghbishi mwingine ni
Mwenyekiti wa kitongoji cha Bujika, Adam Joseph yeye alijiunga na uraghbishi
mwezi Septemba 2015, kwa kutumia nafasi yake uwenyekiti alitambulisha
uraghbishi kwenye kitongoji chake.
“Cha kwanza
nilichofanya ni kuongea na mtendaji wa kijiji na kukubaliana tunahitaji kufanya
hamasa kwa vijana ili wawe wanafika katika mikutano ya vijiji. Hivyo nikaanza
kupita kwenye vijiwe na kuwahamasisha vijana waweze kufika mikutanoni. Na
tuliwalenga vijana wote wa kike na wa kiume,” anaelezea Adam.
Vijana walimwambia
mwenyekiti wao kwamba wao hawasikilizwagi wakija kwenye mikutano na hivyo
hawaoni umuhimu wa kuja kwenye mikutano ya vijiji. Majibu haya yalimpelekea
mwenyekiti kuitisha mkutano uliowausisha vijana na wazee kwa pamoja.
“Nimeshaitisha mikutano
miwili, muamko bado si mkubwa sana kwani bado vijana hawaoni umuhimu wa
kushiriki mikutano hii. Lakini hili halinikatishi tamaa najua hapa ni mwanzo
tu,” anaelezea Adam.
Kwa hakika hizi ni
harakati za kweli katika kumwezesha mwanamke na jamii kwa ujumla. Waraghbishi
kwa pamoja wanakili kwamba uraghbishi ni falsafa ya kutenda. Swali la msingi
kwetu sote, je na sisi tunatenda na kama ndio tunatumia falsafa gani.
CHANZO; MWANAHARAKATI MZALENDO
Post a Comment