Timu za Azam FC, Simba SC, Yanga zimeungana na timu zingine saba kufuzu kwa hatua ya 16 Bora ya michuano ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) mzunguko wa nne utakaochezwa mwishoni mwa mwezi Februari, huku michezo mine ikichezwa leo katika viwanja mbalimbali nchini.
Jumla ya michezo 10 mpaka sasa imeshachezwa na timu kumi kujikatia tiketi ya kucheza mzunguko wa nne, ambao utazikutanisha jumla ya timu 16 mwezi ujao kusaka timu nane zitakazosonga mbele hatua ya nane bora (Robo Fainali).
Timu zilizofuzu hatua ya 16 bora mpaka sasa ni Azam FC, JKT Mlale, Mwadui FC, Ndanda FC, Panone FC, Rhino Rangers, Simba SC, Tanzania Prisons, Toto Africans na Young Africans.
Leo michezo minne itachezwa, Mtibwa Sugar v Abajalo (Jamhuri – Morogoro), Geita Gold v Mgambo Shooting (Nyankumbu – Geita), Lipuli FC v JKT Ruvu (Wambi – Mafinga), na African Sports v Coastal Union (Mkwakwani – Tanga).
Bingwa wa michuano ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) mwaka huu, ataiwakilisha Tanzania mwaka 2017 kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika (CAF-CC)
Post a Comment