Wanafunzi
John Method (kushoto) na Edwin Luguku (wa pili kulia) kutoka Shule ya Sekondari
Mzumbe mkoani Morogoro wakipokea hati zao za ufadhili kutoka kwa Karimjee na
Ofisa Ubalozi wa Ireland nchini, Bi. Carlo. Wanafunzi hao waliibuka washindi wa
jumla katika maonesho ya Sayansi kwa Shule za Sekondari mwaka 2015
yanayoandaliwa na taasisi ya Young Scientists Tanzania (YST). (Picha zote na
Daniel Mbega wa www.brotherdanny.com).
Ofisa
Ubalozi wa Ireland nchini, Bi. Carlo, akizungumza na Edwin Luguku na John
Method kutoka Shule ya Sekondari Mzumbe, Morogoro ambao waliibuka washindi wa
jumla katika maonesho ya Sayansi kwa Shule za Sekondari mwaka 2015
yanayoandaliwa na taasisi ya Young Scientists Tanzania (YST). Wanafunzi hao
wanaondoka leo hii kwenda Dublin, Ireland kwa maonesho ya sayansi.
Mkurugenzi
Mtendaji wa taasisi ya Young Scientists Tanzania (YST), Dk. Gozibert Kamugisha,
akizungumza wakati wa kukabidhiwa kwa scholarship kwa wanafunzi Edwin Luguku na
John Thomas wa Shule ya Sekondari Mzumbe ambao walikuwa washindi wa jumla
katika maonesho ya sayansi 2015. Wanafunzi hao walipewa scholarship hizo la
taasisi ya Karimjee Jivanjee Foundation ya jijini Dar es Salaam.
Meneja wa taasisi ya Karimjee Jivanjee Foundation, Devota Rubama, akizungumza kabla ya kukabidhi hati za ufadhili kwa wanafunzi Edwin Luguku na John Thomas wa Shule ya Sekondari Mzumbe, Morogoro walioshinda katika maonesho ya sayansi 2015.
Mzee Karimjee, Mwenyekiti wa Taasisi ya Karimjee Jivanjee Foundation.
Toyota
Tanzania Limited nao waliwazawadia vijana hao kwa ushindi walioupata.
Na Daniel Mbega wa brotherdanny.com
TAASISI ya
Karimjee Jivanjee Foundation ya jijini Dar es Salaam leo hii imekabidhi
scholarship kwa wanafunzi wawili wa Shule ya Sekondari Mzumbe, Morogoro, ambao
waliibuka washindi wa jumla katika Maonesho ya Tano ya Sayansi ya YST kwa Shule
za Sekondari Tanzania Agosti 2015.
Wanafunzi
hao, Edwin Luguku na John Method, ambao leo hii wanakwenda jijini Dublin,
Ireland kuhudhuria Maonesho ya 53 ya Sayansi, waliibuka washindi kutokana na
utafiti wao wa sayansi usemao “Madhara ya Matumizi ya Mifuko ya Plastiki
Tanzania na Namna ya Kupunguza Matumizi hayo” (The Effects of Using Plastic
Bags in Tanzania and How to Reduce the Same).
Kutokana
na udhamini huo, wanafunzi hao wawili ambao wanatarajia kumaliza kidato cha
sita mwaka huu, watasomeshwa na taasisi hiyo chuo kikuu huku wakilipiwa ada
pamoja na gharama nyingine zote kwa miaka yote watakayokuwa wanachukua shahada
zao.
Itakumbukwa
kwamba, Taasisi ya Karimjee Jivanjee mbali ya kutoa scholarship kwa wanafunzi
hao, pia ilitoa ufadhili kwa shahada ya kwanza chuo kikuu kwa wanafunzi Petro
Samson Ndegeleki na Juma Joshua Wiliam kutoka Nassa Sekondari ya Simiyu ambao
utafiti wao ulihusu ‘How Different Natural Fertilizers Affect the Growth Of
Maize’.
Washindi
hao pia wanaondoka leo hii kwenda Dublin, Ireland kuhudhuria maonesho ya
sayansi ya 53 maarufu kama BT YSTE.
Aidha,
taasisi hiyo, ambayo ilianza kudhamini maonesho hayo tangu mwaka 2012, pia
iliwazawadia washindi wa pili wa jumla ambao ni Emmanuel Lemalali na Emmanuel
Sanga kutoka Tanga Technical na utafiti wao wa ‘A Simple Method For Controlling
Ecto-parasites’.
Meneja wa
taasisi hiyo, Devota Rubama, amesema kwamba taasisi hiyo imejikita katika
kusaidia huduma za kijamii hususan elimu, ambapo kwa mwaka 2015 ilitenga kiasi
cha Shs. 1 bilioni huku akiahidi kwamba, kwa mwaka 2016 wametenda Shs. 1.5
bilioni.
“Tumedhamiria
kuwahamasisha wanasayansi chipukizi wa Tanzania ili kukuza vipaji vyao ili
kulisaidia taifa,” alisema.
Akaongeza:
“Tangu mwaka 2015 hadi sasa tumetoa ufadhili kwa wanafunzi 15 ambao walikuwa
washindi wa jumla na kila mwaka hutoa ufadhili kwa wanafunzi wanne wanaoshinda
katika maonesho ya YST. Wanafunzi walionufaika na ufadhili huo ni watatu kutoka
Kibosho Sekondari (2012), wawili kutoka Ilongelo Sekondari, Singida na wawili
kutoka Fidel Castro, Pemba (2013), wawili kutoka Lumumba Sekondari, Unguja na
wawili kutoka Ngongo Sekondari, Lindi (2014) na sasa tunatoa kwa wawili kutoka
Mzumbe na wawili Nasa, Simiyu walioshinda mwaka 2015.”
Rubama
alisema kwamba taasisi yake ina mpango wa kuanzisha ufadhili wa shahada ya
uzamili kuhusu Uhifadhi Afrika (African Conservation) katika Chuo Kikuu cha
Glasgow, Scotland na Chuo Kikuu cha Nelson Mandela, Arusha ambapo wanufaika
watakuwa watatu kila mwaka ambao watasoma mihula miwili Glasgow na mihula nane
watamalizia Chuo Kikuu cha Nelson Mandela.
“Taasisi
imekwishaanza kutoa ufadhili kwa shahada ya uzamili ya udaktari kuhusu
Paediatric Oncology katika Chuo Kikuu cha Muhimbili ambapo madaktari wawili
walihitimu mwaka 2015 na mwingine atapatiwa ufadhili mwaka 2016.
Katika
maonesho hayo ya 5 yaliyoandaliwa na taasisi ya Young Scientists Tanzania (YST)
kwa mwaka 2015 yalishirikisha jumla ya shule 240 na walimu 120 kutoka shule 120
nchini kote ambapo zawadi mbalimbali zilitolewa kwa washindi zikiwemo fedha
taslimu, medali, vikombe, vifaa vya maabara pamoja na maktaba.
Dk. Gozibert
Kamugisha, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji na Mwanzilishi Mwenza wa YST, ameishukuru
taasisi hiyo pamoja na Serikali ya Ireland kupitia Shirika la Kimataifa la
Misaada la Irish Aid na kuomba wadau wengine wajitokeze kufadhili maonesho
hayo.
(Imeandaliwa na www.brotherdanny.com)
Post a Comment