Meya mstaafu wa Manispaa ya Kinondoni Yusufu Mwenda akijumuika pamoja katika chakula cha pamoja na watoto hao wanaolelewa katika kituo cha Maunga kilichopo Kinondoni Hananasifu Jijini Dar es salaam . |
ILI watoto yatima na wale wanaoishi katika
mazingira magumu waweze kutimiza ndoto zao za kimaisha , Meya mstaafu wa
Manispaa ya Kinondoni Yusufu Mwenda ameiasa jamii kujenga utamaduni wa
kutembelea vituo vinavyowalea watoto hao sanjari na kutatua changamoto
wanazokabiliana nazo hatua itakayowasaidia kufikia malengo hao.
Ametoa rai hiyo
juzi mara baada ya kujumuika pamoja katika chakula cha pamoja na watoto hao
wanaolelewa katika kituo cha Maunga kilichopo Kinondoni Hananasifu Jijini Dar
es salaam ambapo pia alitoa misaada mbalimbali ya yakiwemo madaftari, kalamu,
sabuni,vyakula na fedha kwa ajili ya kusaidia mahitaji ya kituo hicho.
Alisema
watoto yatima na wale wanaoishi katika mazingira magumu wanapaswa kupata elimu
kama ilivyo kwa watoto wengine wanaoishi na wazazi wao hivyo ni jukumu la kila
mwananchi kuona umuhimu wa kutoa chochote alichonacho ili kuwawezesha watoto
hao kuipata elimu hiyo kwa ukamilifu.
“Tunashukuru kwa sasa Rais John Magufuli
ametoa unafuu wa elimu bure kwa watoto katika ngazi ya msingi na Sekondari kwa
hiyo kilichopo hapo ni mahitaji madogo madogo ili kumfanya mtoto aweze kufika
shuleni na kuudhuria masomo, kama jamii hili ni jambo linalowezekana kabisa
tukalitatua kama kila mmoja wetu atakuwa na nia” alisema Mwenda
Aidha katika
hatua nyingine Mwenda ameahidi kutoa huduma ya mahitaji ya shule kwa watoto
wanaosoma darasa la sita hadi sekondari waliopo katika kituo hicho ili
kukipunguzia mzigo kituo hicho katika suala linalohusiana na masomo Mbali na
hilo pia ameahidi kununua vitanda kwa ajili ya watoto hao na kuvifanyia
ukarabati vitanda vilivyoharibika baada ya kuombwa na uongozi wa kituo hicho
kutatua tatizo hilo lililodumu kwa muda mrefu kituoni hapo.
Kwa upande wake
Mlezi wa kituo hicho Zainabu Maunga alisema dhumuni la kuanzishwa kwa kituo
hicho chenye jumla ya watoto 50, lilikuwa kutoa msaada wa malezi kwa watoto hao
waliopatikana kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ya vifo vya wazazi wao.
Alisema kituo hicho kinalea watoto hao wakiwemo wavulana 26 na wasichana 24 kwa
kutegemea misaada ya watu mbalimbali wanaofika kituoni hapo huku akitaja
changamoto mbalimbali wanazokutana nazo katika malezi ya watoto hao.
Alizitaja
changamoto hizo kuwa ni pamoja na ufinyu wa eneo la kituo, mavazi kwa watoto,
chakula pamoja na huduma za afya pale inapotokea mtoto kaugua hatua inayomfanya
kupaza sauti yake kwa jamii kila siku akiomba imsaidie kutatua changamoto hiyo.
MWISHO
MWISHO
Post a Comment