Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Saccos Duniani, Stellah Mtayabarwa (kushoto), akimwelekeza jambo Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Dk. Florens Turuka (kulia), alipotembelea banda la Saccos la Mamlaka ya Bandari (PTA), katika ufunguzi wa maadhimisho hayo uliofanyika viwanja vya Mnazi Mmoja Dar es Salaam leo.
Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Akiba na Mikopo Tanzania (SCCULT), Benard Kalinga (katikati), akihutubia wakati wa ufunguzi wa maadhimisho hayo. Kulia ni Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Dk. Florens Turuka na kushoto ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya maadhimisho hayo, Stellah Mtayabarwa.
Katibu Mkuu wa Shirikisho hilo, Habibu Mhezi (kulia), akizungumza kwenye mkutano huo. Kushoto ni Mwakilishi wa Kamanda wa Polisi wa Kanda ya Dar es Salaam, Mrakibu wa Polisi (SP), Scholastica Luhamba.
Mjasiriamali Zamda Sasillo (kushoto), akiwa na wateja walitembelea banda lake katika maadhimisho hayo. Kutoka kulia ni Magdalena Samkumbi, Lubanzo Kalufya na Ashura Shoka.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Dk. Florens Turuka (kulia), akizungumza na Ofisa Uendeshaji Mkuu, Mfuko wa Pembejeo, Pili Mogasa.
Ofisa Masoko wa Mfuko wa Pensheni wa PPF, akitoa maelezo kwa Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Dk. Florens Turuka (kulia), kuhusu shughuli mbalimbali zinazofanywa na mfuko huo.
Ofisa Masoko wa Benki ya Posta Tanzania, Ezekiel Fumbo (kushoto), akimuelekeza Dk. Turuka kazi mbalimbali zinazofanywa na benki hiyo.
Viongozi Meza kuu wakipiga makofi wakati wakipokea maandamano ya maadhimisho hayo.
Wadau wakiwa kwenye maadhimisho hayo.
Wasanii wa Kikundi cha Utamaduni cha Sanaa cha Magereza kikitoa burudani kwenye hafla hiyo.
Wasanii wa Kikundi cha Utamaduni cha Sanaa cha Magereza kikionesha umahiri wa kucheza ngoma aina ya chaso inayochezwa na wenyeji kutoka Pemba.
Hapa ni mserebuko wa ngoma ya chaso ya wenyeji wa Pemba.
Na Dotto Mwaibale
SERIKALI imesema itaendelea kushirikiana na vyama vya akiba na mikopo ili kujenga mazingira bora ya kuinua uchumi nchini.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk. Florens Turuka wakati wa ufunguzi wa Siku ya Saccos duniani uliofanyika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam leo.
"Vyama vya akiba na mikopo ni wadau wakubwa wa serikali kwani vinasaidia sana katika kiinua uchumi wa nchi hivyo hatuna budi kuendelea kushirikiana" alisema Dk.Turuka.
Dk. Turuka aliwataka viongozi wa vyama hivyo kumaliza changamoto zao wao wenyewe na wanachama wao pale zinapotokea badala ya kukimbilia serikalini.
Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Akiba na Mikopo Tanzania (SCCULT), Benard Kalinga alisema vyama hivyo vimepata mafanikio makubwa kwani wamefanikiwa kuanzisha Saccos 4,000 ambazo zipo hadi vijijini na kuwa na wanachama milioni 1.5 nchini.
"Sheria namba sita ya vyama vya ushirika ya mwaka 2013 imeanza kutumika baada ya kupata idhini ya Rais mwezi Oktoba 2013 lakini ni dhahiri kuwa kumekuwa na malalamiko mengi juu ya baadhi ya maeneo yaliyoko kwenye sheria hiyo" alisema Kalinga.
Alisema licha ya kupata mafanikio hayo changamoto kubwa waliyonayo ni ushirikishwaji wa kuandaa sheria inayoongoza vyama vya ushirika nchini.
Post a Comment