Mchuano mkubwa katika uchaguzi huu ni kati ya Donald Trump wa Chama cha Republican na Hillary Clinton wa Chama cha Democratic. Wagombea hawa wamekuwa wakipambana vikali kwenye majukwaa na midahalo wakieleza ni namna gani wataiongoza Marekani na pia ni jinsi gani kila mmoja akimuelezea mwenzake kuwa hafai.
Kikubwa cha kuweza kufahamu katika uchaguzi mkuu wa Marekani ni mfumo unaotumiwa kumpata rais wa nchi hiyo. Tofauti na mfumo wa uchaguzi wa nchi nyingi, Rais wa Marekani hachaguliwi kutokana na kura nyingi alizozipata kutoka kwa wananchi (First past the post).
Marekani inatumia mfumo unaofahamika kama ‘Electoral College’ ambao ni kundi la watu (wawakilishi) wanaochaguliwa kutoka kila jimbo kumchagua Rais na Makamu wa Rais wa Marekani baada ya wananchi kupiga kura.
Wananchi wanapopiga kura hawamchagui rais moja kwa moja lakini badala yake wanachagua kundi la watu (wawakilishi) watakaokwenda kupiga kura zitakazoweza kuamua mshindi wa kinyang’anyiro.
Jinsi ya kutambua idadi ya wawakilishi watakaomchagua rais kutoka kwenye kila jimbo hutegemea na idadi ya watu wanaoishi katika jimbo hilo. Hii ina maana kuwa kama jimbo lina watu wengi, litapata nafasi ya kutoa wawakilishi wengi watakaomchagua rais, mfano, jimbo la California lenye wakazi milioni 38.8 litatoa wawakilishi 55 wakati jimbo la Delaware lenye wakazi 936,000 litatoa wawakilishi 3.
Inawekezana mgombea wa upande mmoja akapata kura nyingi kutoka kwa wananchi (Popular votes) lakini akashindwa katika kura za wawakilishi (Electoral College votes). Katika uchaguzi wa mwaka 2000, Rais Mstaafu George W. Bush alitangazwa kuwa rais licha ya kuwa hakushinda katika kura zilizopigwa na wananchi. Bush alipata kura 50,456,002 huku mpinzani wake Al Gore akipata kura 50,999,897 lakini kwenye kura za wawakilishi (Electoral College Votes) Bush alipata kura 271 huku Al Gore akipata kura 266.
Huu ni mgawanyiko wa kura za wawakilishi kutoka kila jimbo nchini Marekani.
Kwa sasa kuna wawakilishi (wanaomchagua rais na makamu wa rais) ni 538 ambao 435 ni wawakilishi katika Bunge la Marekani, 100 ni Maseneta pamoja na wawakilishi wengine watatu kutoka wilaya ya Columbia.
Mgombea wa kwanza kufikisha jumla ya kura 270 kutoka kwa wawakilishi hawa ndiye anakuwa ameshinda kiti cha urais wa Marekani.
Mfumo huu wa uchaguzi ulianzishwa nchini marekani ili kuhakikisha kuwa hakuna uwezekano wa kikundi cha watu kuushawishi umma hata kwa uongo ili waweze kushinda uchaguzi.
Post a Comment