Na JOVINA BUJULU- MAELEZO
Novemba
Tano mwaka huu ni mwaka mmoja tangu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli alipoapishwa kuwa kiongozi na
Amri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama wa Nchi hii.
Katika
kipindi cha mwaka mmoja wa uongozi wake, Watanzania wameshuhudia
mafanikio makubwa katika katika sekta ya ukusanyaji kodi kupitia vyanzo
mbali mbali vya mapato.
Hatua
hii inatokana na kuwa Rais Magufuli alipoingia madarakani amekuwa
mstari wa mbele kuhakikisha hakuna mfanyabiashara anayekwepa ulipaji
kodi na kuwahimiza wananchi kuhakikisha wanadai risiti kwa kila bidhaa
au huduma wanayolipia.
Hivyo
Serikali hii tangu ianze kazi rasmi imekuwa ikitilia mkazo ukusanyaji
wa mapato ya Serikali kwa kuziba mianya ya upotevu wa mapato na kubuni
vyanzo vipya ili kuongeza makusanyo ya Serikali.
Juhudi
hizi za Rais Magufuli za kuongeza mapato na kudhibiti upotevu wa mapato
ya Serikali zimejionyesha katika mikutano yake mingi ambapo mara nyingi
amekuwa akisema “Ukinunua bidhaa dai risiti na ukiuza bidhaa toa
risiti”.
Jitihada
hizo za wa ukusanyaji wa kodi kwa ajili ya kuongeza mapato ya Serikali
kwa manufaa zitatekelezwa na uongozi wa Rais Magufuli zinaunga mkono
wosia aliwahi kuutoa Baba wa Taifa hili Mwalimu Julius Kambarage Nyerere
ambapo alisema kuwa “Serikali yeyote isiyokusanya kodi ni “corrupt”.
Hatua
hiyo ya kutoa na kudai risiti ina mchango mkubwa kwa serikali katika
kukusanya kodi ambazo zitasaidia katika kuboresha huduma za jamii kama
vile elimu, afya, maji, umeme, usafirishaji, ujenzi na uendeshaji wa
serikali kwa ujumla kutokana na mapato yanayopatikana.
Hapa
nchini, Mamlaka ya Mapato (TRA) ndicho chombo chenye jukumu la
kusimamia ukusanyaji wa mapato ya Taifa na imekuwa ikitimiza lengo hilo
kwa kutekeleza mikakati mbalimbali kama ilivyoainishwa katika mpango
mkuu wa miaka mitano.
Kwa
mujibu wa Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi Bw. Richard
Kayombo, katika kipindi cha mwaka mmoja wa utawala wa Rais Magufuli
kumekuwepo na ongezeko la makusanyo ya mapato ya serikali yatokanayo na
kodi.
Anasema
kuwa katika kipindi hiki, TRA inakusanya wastani wa trillion 1.1 kila
mwezi kuanzia mwezi Novemba, 2015 hadi Septemba 2016.
“Hili
ni ongezeko la asilimia 28.1 kutoka kwenye kukusanya wastani wa
shilingi bilioni 867 kwa mwezi katika kipindi cha mwezi Novemba, 2014
hadi Septemba 2015” anasema Bw. Kayombo.
Makusanyo
ya mapato katika kipindi cha utawala wa Rais Magufuli kuanzia mwezi
Novemba 2015 yamekuwa yakiongezeka ikilinganishwa na miaka iliyotangulia
kwa mfano mwaka wa fedha 2015/2016 mapato yaliyokusanywa yalikuwa
shillingi trilioni 12.5 ikiwa ni ongezeko la asilimia 26.4 ya makusanyo
ya mwaka 2014/2015.
Aidha
TRA imekwisha kusanya kodi kiasi cha shilingi trilioni 3.5 kufikia
mwezi Septemba 2016, ikiwa ni ongezeko la asilimia 23.4 ikilinganishwa
na kipindi kama hiki cha robo mwaka 2015/16.
Bw.
Kayombo anaongeza kuwa kwa sasa TRA inatekeleza mpango mkakati wa nne
wa ukusanyaji kodi wenye dhamira ya kuongeza makusanyo ya kodi za ndani
kwa kuongeza ulipaji kodi wa hiari.
“Jitihada
mojawapo zinazofanywa na TRA ni pamoja na kuboresha mifumo ya makusanyo
inayoendana na mazingira ya sasa ya ukuaji wa teknolojia ili
kuhakikisha walipa kodi wanalipa kwa urahisi kama ilivyo dhamira yake ya
kurahisisha ulipaji kodi na kufanya mazingira yawe bora” anasema Bw. Kayombo.
Katika
kipindi cha mwaka mmoja ambao Rais Magufuli amekuwa madarakani, juhudi
mbalimbali zimefanyika ili kuhakikisha matarajio ya Rais ya kuimarisha
makusanyo ya kodi na kudhibiti mianya ya rushwa yanafanikiwa.
Mafanikio
hayo yatamuwezesha Rais Magufuli kutimiza ahadi zake alizozitoa wakati
wa kampeni zikiwemo kuboresha afya, upatikanaji wa maji, umeme, kutoa
elimu bure, ujenzi wa miundombinu kama vile viwanja vya ndege, reli na
barabara.
Aidha
makusanyo hayo yatawezesha uwekezaji katika ujenzi wa viwanda ambavyo
vitatoa ajira kwa wananchi na serikali kuweza kujitegemea na hivyo
kupunguza utegemezi wa misaada kutoka kwa wafadhili.
Bw.Kayombo
anataja kiini cha ongezeko la kukusanya kodi kuwa ni matumizi ya
mashine za kielektroniki (EFD) ambazo zinatumika zaidi badala ya
stakabadhi zinazoandikwa kwa mkono.
“Matumizi
ya stakabadhi zinazoandikwa kwa mkono hayakuwa na ubora mzuri wa
kukusanya na kuongeza mapato na kutunza kumbukumbu sahihi ambayo
yaliifanya serikali ipoteze mapato mengi” anaongeza.
Katika
hatua nyingine TRA ilitoa mashine za EFDs 130 bure kwa makatibu wakuu
wa Wizara mbali mbali kwa ajili ya taasisi za serikali ambazo
zinakusanya maduhuli ya serikali kwa nia ya kudhibiti upotevu wa mapato
ya serikali.
Katika
kuhakikisha makusanyo ya kodi yanaongezeka TRA imeendelea kudhibiti
mianya ya ukwepaji kodi, kufichua wakwepa kodi, kupambana na rushwa na
kupanua wigo wa kodi kwa kusajili wafanyabiashara ambao hawajasajiliwa
sambamba na kuendesha zoezi la kuhakiki namba ya utambulisho wa mlipa
kodi (TIN) linaloendelea jijini Dar es Salaam kwa sasa ili kuboresha
daftari la walipa kodi.
Pamoja
na mafanikio hayo Kayombo alizitaja changamoto wanazokutana nazo katika
ukusanyaji kodi kuwa ni pamoja na taarifa za kodi kutowafikia wananchi
wote ili kujenga uhiari wa kulipa kodi na uwepo wa ukanda mrefu wa Pwani
unaosababisha kuwepo mianya mingi ya ukwepaji kodi ambapo bidhaa
huingizwa nchini kwa njia za panya.
Pamoja
na changamoto hizo, Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) imeendelea kubuni
mikakati mbali mbali ya kuongeza ukusanyaji wa mapato ili kuendana na
kauli mbiu ya serikali ya awamu ya tano isemayo “HAPA KAZI TU” ili
kutimiza na kuvuka lengo la kukusanya shilingi trilioni 15.1 kwa kipindi
cha mwaka wa fedha 2016/17.
Post a Comment