Na Benny Mwaipaja, WFM, Dar es salaam
Wizara
ya Fedha na Mipango imekamilisha ujenzi wa mfumo wa malipo moja kwa
moja kupitia akaunti za walipwaji katika mtandao wa malipo wa Benki Kuu
ya Tanzania (Tanzania Interbank Settlement System – TISS), katika mkoa
wa Morogoro, hatua inayolenga kuongeza ufanisi wa miamala mbalimbali
inayofanywa na serikali
Katibu
Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dotto James amezitaja Halmashauri
ya Manispaa ya Morogoro, Halmashauri za Wilaya ya Kilombero, Morogoro,
Mvomero, Kilosa na Ulanga, kwamba zitaanza kufanya malipo hayo kwa mfumo
huo wa TISS kuanzia mwezi Desemba mwaka huu.
“Nia
ya Serikali ni kuhakikisha kwamba ifikapo mwezi Desemba, 2016
Halmashauri zote zilizopo katika Mkoa wa Morogoro ziweze kufanya malipo
kwa kutumia mfumo wa malipo wa TISS” alisema Dotto James.
Amesema
kuwa malipo hayo yatafanyika kwa kutumia mfumo wa malipo wa TISS
uliojengwa katika mikoa yote Tanzania Bara ikiwemo Ofisi za Hazina Ndogo
na Sekretariati za Mikoa, Wizara, Idara za Serikali zinazofanya malipo
yake kupitia Ofisi Kuu ya Malipo (CPO) iliyopo Hazina, malipo ya
Pensheni kwa wastaafu, Kitengo cha Kupambana na Fedha Haramu, Mfuko wa
Bunge, Mfuko wa Mahakama na Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi.
“Hivi
karibuni mfumo huu wa malipo umeunganishwa katika Halmashauri ya Jiji
la Dar es salaam, Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, Kinondoni na Temeke.
Katika Halmashauri ya Jiji la Mwanza, mfumo huu umeunganishwa katika
Halmashauri za Wilaya ya Ukerewe, Magu, Sengerema, Kwimba, na Misungwi”
alifafanua Katibu Mkuu huyo.
Ameongeza
kuwa katika mkoa wa Mbeya, mfumo huo umefungwa katika Halmashauri ya
jijini la Mbeya, Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe, Kyela, Mbarali,
Chunya, Mbeya, Mbozi na Ileje wakati mkoani Arusha maeneo yanayohusika
ni Halmashauri ya Jiji la Arusha, Halmashauri ya Wilaya ya Arusha,
Longido, Meru, Monduli, Karatu, Ngorongoro.
Halmashauri
ya Manispaa ya Dodoma mfumo huu umeunganishwa katika Halmashauri ya
Wilaya ya Bahi, Kongwa, Mpwapwa, Chamwino, na Kondoa wakati mkoani
Tanga, Halmashauri ya Jiji la Tanga, Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga,
Pangani, Muheza, Handeni, Kilindi, Korogwe, Lushoto na Mji wa Korogwe
zimeunganishwa katika mfumo huo.
Kuanzia
Julai, 2010 hadi katikati ya Mwezi Novemba, 2016 mfumo huu ulikuwa
tayari umeunganishwa katika Serikali Kuu na Mamlaka za Serikali za Mitaa
zilizopo katika Mikoa ya Dar es salaam, Mwanza, Mbeya, Songwe, Arusha,
Dodoma na Tanga ambapo umeonesha mafanikio makubwa” Alisema Bw. Dotto
James.
Katibu
Mkuu huyo amewataka wadau wote wanaofanya biashara na maeneo
yaliyofungwa mfumo huo mkoani Morogoro, kuwasilisha taarifa muhimu ili
ziweze kuingizwa katika Mtandao wa malipo wa Serikali [Intergrated
Financial Management System (IFMS)] ili uanze kutumika kuanzia Mwezi
Desemba mwaka huu kufanya malipo.
Taarifa
hizo zinahitajika kwa kuwa ni muhimu ili kuwezesha malipo kufanyika kwa
mlipwaji, ikiwa ni pamoja na Namba ya akaunti ya benki, Namba ya tawi
la benki, Jina la akaunti, Aina ya akaunti, Namba ya kuandikishwa
biashara, Namba ya kuandikishwa Kampuni, Namba ya Mlipakodi, Jina la
benki na Jina la Tawi la benki.
“Hivyo
Makampuni na watu wanaofanya biashara na Halmashauri ya Manispaa ya
Morogoro, Halmashauri za Wilaya ya Kilombero, Morogoro, Mvomero,
Kilosa, na Ulanga wanashauriwa kuwasiliana na Halmashauri husika ili
waweze kupatiwa fomu maalum za kujaza taarifa hizo muhimu” Alisisitiza
Dotto James.
Amesema
kuwa zoezi hilo ni endelevu ambapo Serikali itaendelea kufunga mfumo
huo kwenye mikoa na Wilaya zote zilizobaki upande wa Tanzania Bara.
Post a Comment