MAMLAKA
ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imepokea maombi kutoka
Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) ya kupandisha gharama za umeme kwa
asilimia 18.19 kuanzia mwaka ujao.
Taarifa
iliyotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa wa Huduma za Nishati na Maji
(Ewura) imeeleza kuwa Oktoba 4, mamlaka hiyo ilipokea ombi la mabadiliko
ya bei ya umeme, hivyo unaandaliwa mkakati wa kukusanya maoni ya wadau
wa nishati hiyo.
“Mikutano
ya ukusanyaji maoni kuhusu bei inayopendekezwa na Tanesco itaanza
Novemba 16 katika mikoa ya Mwanza, Mbeya, Arusha, Dodoma na kwa Dar es
Salaam ni Novemba 23,” inaeleza taarifa hiyo.
Aprili
mwaka huu, Tanesco ilituma maombi kwa Ewura ya kupunguza gharama za
umeme kwa asilimia 1.1, lakini baada ya mamlaka hiyo kupitia maombi
hayo, ilipunguza gharama hizo kwa asilimia 1.5 hadi 2.4.
Bei
ya sasa baada ya punguzo hilo la Ewura kwa wateja wa shirika hilo,
kutoka kundi la D1 wanaotumia kiasi cha umeme kuanzia kilowati 0 hadi 75
ni Sh 100 na zaidi ya kilowati 75 kwa mwezi wanatozwa Sh 350 kwa uniti
moja.
Aidha,
kwa wateja wa kundi la T1 ambao ni kuanzia majumbani, viwandani na
biashara ndogo ndogo hutozwa kiasi cha Sh 292 kwa uniti moja na kwa
wateja wa kundi T2 ambalo ni kundi linalotumia umeme kuanzia kilowati
7,500 hutozwa kwa wastani wa Sh 15,004 kwa mwezi kwa uniti moja.
Kwa
makundi ya T3 na T4 wanaotumia umeme mkubwa kama vile kwenye machimbo,
viwanda vikubwa na Mamlaka ya Umeme Zanzibar (ZECO) yenyewe hutozwa
kiasi cha Sh 13,200 hadi 16,550 kwa mwezi kwa uniti moja.
Hata
hivyo, kutokana na ombi hilo la ongezeko la bei kwa asilimia 18.19,
sasa wateja wa kawaida wanaotumia umeme kuanzia kilowati hadi 75
watakuwa na ongezeko la Sh 18 ambapo endapo ombi hilo likiridhiwa
watatozwa Sh 118 kwa uniti moja.
Aidha,
kwa wateja wanaonunua umeme zaidi ya kilowati 75 ambao kwa sasa
wanatozwa Sh 350 kwa uniti moja, endapo ombi hilo likipitishwa watakuwa
na ongezeko la bei la Sh 63 hivyo watatozwa kiasi cha Sh 413 kwa uniti
moja.
Kwa
upande wa wateja wa kundi la T1 ambao ni kuanzia majumbani, viwandani
na biashara ndogo ndogo wanaotozwa kwa sasa kiasi cha Sh 292, watakuwa
na ongezeko la Sh 52.56 hivyo endapo ombi hilo litaridhiwa bei hiyo
itapanda na kufikia Sh 344.56 kwa uniti moja.
Meneja
Mawasiliano na Uhusiano wa Ewura, Titus Kaguo pamoja na kuthibitisha
mamlaka hiyo kupokea maombi hayo, alisisitiza kuwa bado ombi hilo
linachambuliwa na kufanyiwa tathmini na mamlaka hiyo kabla ya
kuidhinishwa.
Post a Comment