Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya
Taifa ya Uchaguzi (NEC) Bw. Kailima Ramadhani akitoa ufafanuzi kuhusu
masuala mbalimbali juu ya utendaji wa NEC katika kipindi cha Power
Breakfast kinachorushwa na Kituo cha Redio cha Clouds FM mwishoni mwa
wiki jijini Dar es salaam.
Na Margareth Chambiri – Dar es salaam.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya
Taifa ya Uchaguzi (NEC) Bw. Kailima Ramadhani amesema jambo kubwa
ambalo watanzania wanapaswa kujifunza kutokana na Uchaguzi wa Marekani
uliomalizika hivi karibuni ni kwa wananchi kuheshimi mifumo ya Uchaguzi.
Mkurugenzi Kailima ametoa kauli
hiyo ikiwa ni tathimi yake kuhusu uchaguzi huo wa Marekani na namna
ambavyo baadhi ya watu wamekuwa wakihoji kuhusu ucheleweshaji wa
kutangaza matokeo ya uchaguzi unaofanywa na Tume ikilinganishwa na
ilivyofanyika nchini Marekani.
Akizungumza mwishoni mwa wiki
katika kipindi cha Power Breakfast kinachorushwa na Kituo cha Redio cha
Clouds FM, Kailima amesema siyo sahihi kulinganisha uchaguzi wa Marekani
na Tanzania, akitolea mfano sekta ya mawasiliano ambayo ni muhimu
katika kusafirisha vifaa na taarifa mbalimbali za uchaguzi
inavyokabiliwa na changamoto.
Amesema watanzania na hasa Wapiga
kura wengi wanaishi maeneo ya vijijini ambayo baadhi yake hayafikiki
kwa urahisi na kwamba haiwezekani Tume ikatangaza matokeo bila
kuhakikisha kuwa kila kura imehesabiwa ikiwemo ya yule mwananchi wa
kijijini.
Amebainisha kuwa yapo mambo ya
msingi ambayo watanzania wanapaswa kujifunza kutokana na Uchaguzi wa
Marekani, kubwa ikiwa ni hatua ya kuheshimu mifumo ya Uchaguzi sambamba
na Mamlaka zinazosimamia chaguzi hizo.
Ametolea mfano wa uvumilivu
katika kusubiri matokeo na Wagombea kuheshimu matokeo yanayotangazwa na
Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa mujibu wa sheria kwani hata pale ambapo
anayeshindwa hakuridhika bado anaweza kupinga matokeo kwa kufuata
taratibu zilizopo kisheria.
Katika hatua nyingine Mkurugenzi
huyo amesema Tume ya Taifa ya Uchaguzi inakamilisha Mwongozo wa Utoaji
wa Elimu ya Mpiga Kura wa 2015-2020 ili iweze kuzishirikisha Asasi za
Kiraia, Taasisi au Vikundi mbalimbali vya Watu wanaotaka kutoa Elimu
hiyo.
Kwa mujibu wa Bwana Kailima Tume
imo katika hatua za mwisho za kupitia Rasimu ya Mwongozo wa Elimu ya
Mpiga Kura kwa ajili ya kuupitisha uweze kutumiwa na Wadau mbalimbali wa
Uchaguzi.
Amesema pamoja na hatua ya Tume
ya kuanza kutoa Elimu ya Mpiga Kura mapema kuliko ilivyozoeleka na
wananchi, inakusudia kupanua zaidi wigo wa utoaji wa Elimu hiyo kwa
kuwashirikisha wadau wengi zaidi wakiwemo Viongozi wa Dini.
Bwana Kailima amesema Tume
kupitia kwa Mwenyekiti wake Mheshimiwa Jaji (Mstaafu) Damiani Lubuva
baadaye mwezi huu itatoa taarifa rasmi kwa ajili ya kuzialika Taasisi na
Asasi za Kiraia zinazotaka kutoa Elimu ya Mpiga Kura kuwasilisha maombi
yao kwa ajili ya kupatiwa kibali rasmi cha kutoa Elimu ya Mpiga Kura.
Aidha Mkurugenzi huyo wa Uchaguzi
amevitaja vigezo vya kupatiwa kibali kwa ajili ya kutoa Elimu ya Mpiga
Kura kuwa ni pamoja na Cheti cha Usajili, Asasi au Taasisi kuwa imefanya
kazi nchini kwa kipindi kisichopungua miezi sita pamoja na kuwasilisha
majina ya watendaji wa juu wa Taasisi au Asasi husika.
Akizungumzia kuhusu tathmini ya
zoezi hilo linaloendelea kufanywa na Tume yake, Bwana Kailima
Halmashauri amesema limekuwa na mafanikio makubwa na anaamini kwa
kushirikiana na Wadau mbalimbali wa Uchaguzi kutawezesha wananchi wengi
kufikiwa na Elimu hiyo na kwamba Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020 hakutakuwa
na malalamiko na badala yake zoezi la uchaguzi litakuwa rahisi.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi tayari
imeanza utekelezaji wa zoezi la Utoaji wa Elimu ya Mpiga Kura ambapo
imeshiriki katika maonesho mbalimbali yakiwemo ya Biashara ya Kimataifa
na yale ya Wakulima pamoja na kutembelea na kutoa Elimu ya Mpiga Kura
katika shule kadhaa za Sekondari hapa nchini.
Post a Comment