Mbunge wa Mbeya Mjini Joseph Mbilinyi (SUGU) |
Na JamiiMojaBlog,Mbeya
Mkazi wa Iyunga jijini Mbeya ambaye
amefahamika kwa jina moja la Rechal (13) amefariki dunia mara baada ya kugongwa
na gari , namba T161 CPP Toyota LandCruiser inayodaiwa kumilikiwa na Mbunge wa
Jimbo la Mbeya mjini, Joseph Mbilinyi maharufu kwa jina la (SUGU), kwenye
kivuko cha barabara (ZEBRA) na kumsababishia kifo chake papo hapo.
Tukio hilo limetokea leo Desemba 17 majira ya saa mbili asubuhi huko katika eneo
la Iyunga Jijini hapa, wakati gari ya Mbunge huyo ikiwa njiani kuelekea uwanja
wa ndege wa Songwe kwa ajili ya mapokezi ya kiongozi wa Kitaifa Freeman Mbowe.
Imeelezwa kuwa, gari hilo likiwa
katika mwendokasi linadaiwa kukiuka sheria za barabarani kwa kutosimama kwenye
kivuko cha barabara kinachowaruhusu watembea kwa miguu kuvuka na kumgonga mtoto
huyo na kusababisha kifo chake papo hapo.
Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo
wakizungumza , kwa nyakati tofauti , wamesema mtoto huyo akiwa na mama yake
walikuwa wakivuka barabara baada ya magari ya upande wa pili kusimama na
kuwaruhusu watembea kwa miguu hao kuvuka.
Amesema, wakiwa katikati ya kivuko
hicho mama wa marehemu alishangaa kuliona gari ya Mbunge hiyo ikija kwa kasi
hivyo kumuachia mtoto wake aliyekuwa amemshika mkono na yeye kutafuta njia ya
kujiokoa.
Wameeleza kuwa licha ya dereva wa gari ya Mbunge kuona
madereva wenzie wa magari yaliyokuwa yakitokea Mbalizi wakisimama kwa ajili ya
kuwaruhusu watembea hao kuvuka lakini yeye akitokea mjini Mbeya alishindwa
kutii sheria hiyo na kupita akiwa katika mwendo kasi.
“Madereva wenzie tumesimama ili mama
na mtoto wavuke lakini yeye akiwa na haraka alipita tu, kwa kweli hii inauma
sana, nasikia mtoto amepoteza maisha lakini mama amejeruhiwa na kwamba
amekimbizwa hospitali Teule ya Ifisi kwa matibabu,”alisema mmoja wa mashuhuda
hao.
Gari la Mbunge wa Mbeya mjini Mheshimiwa Joseph Mbilinyi (Sugu) Toyota Land Cruser T.161 CPP likiwa ofisi za Usalama barabarani jijini Mbeya baada ya kugonga mtembea kwa miguu na kusababisha kifo . |
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Dhahiri Kidavashari akizungumza
kwa njia ya simu amekiri kutokea kwa tukio hilo na kuthibitisha kifo cha mtoto
huyo.
Aidha Kivadashari ametaja jina la dereva wa gari hiyo kuwa ni Gabriel Endrew alimaarufu Dj BBG (43) mkazi wa
Mwakibete jijini hapa.
Amesema hilo limetokea majira ya saa mbili asubuhi ambapo
gari T161 CPP ilimgonga mtembea kwa miguu ambaye ni mtoto anayekadiriwa miaka
13 ambapo amefahamika kwa jina moja la Rechal na kumsababishia kifo wakati
akikimbizwa hospitali .
Pia, aliongeza kuwa gari hiyo
imekamatwa na dereva anashikiliwa na polisi kwa ajili ya mahojiano na kwamba
polisi wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo.
Mwisho.
Post a Comment