Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limeanza mazungumzo na
Taasisi ya Tiba ya Moyo ya Jakaya Kikwete iliyoko Muhimbili, Dar es
Salaam.
TFF imeanza mazungumzo hayo, ili kwa pamoja waanze kushiriana kutoa
mafunzo kwa madaktari na wahudumu wa afya kwa wanamichezo wa soka katika
kushughulikia matatizo ya moyo.
Ni matumaini yetu kuwa mafunzo haya yataboresha uwezo wa madaktari wa
mpira wa miguu sambamba na kusambazwa kwa vifaa maalumu vya tiba ya
moyo kwenye klabu za soka nchini.
Hii ni hatua thabiti inayochukuliwa na uongozi wa TFF baada ya
kutokea vifo vinavyosababishwa na mshtuko wa moyo kwa wachezaji ukiwamo
ugonjwa wa ‘cardiac arrest’ ambao kwa taarifa za AWALI unaonyesha ndio
uliosababisha kifo cha Mchezaji wa Mbao FC U20, Ismail Mrisho Khalfan.
Marehemu Ismail Mrisho Khalfan alifariki dunia baada ya kuanguka
uwanjani Desemba 4, 2016 kwenye Uwanja wa Kaitaba, Kagera wakati timu
yake ya Mbao ikicheza na Mwadui katika mechi ya ligi ya vijana wenye
umri wa chini ya miaka 20.
Kifo hicho kimegusa hisa za wanafamilia wengi wa mpira wa miguu
akiwamo Rais wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu Ulimwenguni
(FIFA), Bw. Gianni Infantino ambaye juzi alituma salamu za rambirambi
kwa Rais Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Bw. Jamal Emil
Malinzi kutokana na kilo cha ghafla cha Mchezaji.
Salaam Rais Infantino, zinakwenda sambamba na za Waziri wa Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo wa Tanzania, Ndugu Nape Nnauye na Rais wa
Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), Issa Hayatou.
Mchezaji Ismail Mrisho Khalfan wa timu ya vijana wenye umri wa chini
ya miaka 20 wa Mbao FC ya Mwanza, kilitokea Desemba 4, 2016 kwenye
Uwanja wa Kaitaba, Bukoba mkoani Kagera wakati timu yake ikicheza mchezo
huo dhidi ya Mwadui FC ya Shinyanga.
Timu hiyo ya Vijana wa Mbao, kama vilivyo timu nyingine 7 za Ligi kuu
ya Vodacom, ilikuwa Kituo cha Bukoba katika Ligi ya avijana ambayo kwa
msimu huu imefanyika kwa mara ya kwanza. Timu nyingine Nane zilikuwa
kituo cha Dar es Salaam.
Ismail aliyeanguka uwanjani dakika ya 74, alipata huduma ya kwanza
uwanjani hapo kwa madaktari waliokuwa uwanjani, lakini baadaye taarifa
za kitabibu zilionyesha amefariki dunia.
Kamati ya Tiba ya TFF, bado inaendelea na uchunguzi wa kifo cha
mchezaji huyo kabla ya baadaye kutoa taarifa za kamili ya kitatibu kujua
hasa chanzo hasa cha kifo cha mchezaji huyo ambaye mwili wake
umehifadhiwa kwenye Hospitali ya Mkoa Kagera. Marehemu Ismail Mrisho
Khalfan alizikwa Desemba 5, 2016 jijini Mwanza.
…………………………………………………………………………………………………
Post a Comment