Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Mara nyingi wafugaji wanakabiliwa na changamoto kadhaa katika ufugaji wao wa kuku. Changamoto hizo ni pamoja na Visumbufu mbalimbali mfano, Viroboto, Utitiri na chawa. Visumbufu hivi vimekuwa tishio kubwa katika kufanya ufugaji wa kuku uwe wenye tija kutokana na kusababisha vifo vingi.

Katika banda lako la kuku ukivamiwa na wadudu hawa kwa hakika afya ya kuku wako itaanza kuzorota kwa haraka na kuwafanya kuku wako waonekane kama wanaumwa vile. Ni wadudu wanaonyonya damu kwa kiasi kikubwa sana na hivyo kusababisha kuku kufa kwa ugonjwa wa kuishiwa damu mwilini. Lakini vilevile kwa kuku wanaotaga huwafanya washushe utagaji wao ghafla. Ukiwatazama unaweza kuona kama wanaumwa kwa maana wanakonda, kuzubaa na kupoteza hamu ya kula. Muda mwingi wanakuwa wanajisokonyosokonyoa katika manyoya yao kwa kutumia midomo yao. Hii ni kutokana na adha wanayopata hasa kuwashwa na maumivu wanayosababishiwa.

Viroboto ni rahisi kuonekana kwa kuwa wanakaa sehemu za wazi za kuku mfano kuzunguka maeneo ya macho, katika ndevu na mapanga yao nk. Tatizo ni kwa utitili na chawa wenyewe si rahisi kuonekana kama mfugaji siyo mfuatiliaji wa karibu wa kuku wake. Utitiri na chawa wenyewe wanakaa ndani ya manyoya ya kuku kwenye ngozi kabisa. Utitiri ni mdogo kuliko chawa. Chawa wanakuwa weupe hivi wanajishika katika ngozi. Utawaona endapo utapekenyua katika manyoya ya kuku. Wakati utitiri wenyewe unatakiwa uwe na macho mazuri kuweza kuwaona kwa kuwa ni wadudu wadogo zaidi lakini ukipekenyua kwenye manyoya na kufika ndani kabisa kwenye ngozi utawaona wakitembeatembea. Wanapenda kukaa kwenye kwapa ya kuku na kwenye ngozi ya mwili wake

Usipojua vizuri kuhusu visumbufu hivi unaweza ukadhani kuwa kuku wako wanaumwa ugonjwa mwingine kabisa katika magonjwa ya kuku. Na kwamba utahangaika kutumia gharama nyingi ya madawa huku kuku wako wakiendelea kuzorota bila kupata nafuu ya matibabu unayohatumia.

Ni muhimu kabla ya kutibu kuku wako ukawasiliana na mtaalamu wa mifugo aliyekaribu yako ili aweze kukusaidia kukukagulia na kubaini tatizo halisi la kuku wako. Kwa maana kuku hawahitaji mchezo wa kubahatisha. Unatakiwa ujue ni tatizo gani hasa linawakabili kuku wako ili waweze kupatiwa tiba ya uhakika.

Sasa nini kifanyike kama banda lako litakuwa limevamiwa na Visumbufu hivyo?

Kuna dawa nyingi za kutumia, unaweza kutumia Dawa za unga za kunyunyiza mfano Akheri powder au nyingine inaitwa Sevin (Dudu) Dust. Dawa hizi utanyunyiza kuku wako wote mmoja baada ya mwengine kwenye manyoya yao na sehemu zile ambazo zimevamiwa na wadudu hao mfano machoni na kwenye mapanga yao na vilevile utapaswa dawa hizo kunyunyiza kwenye malanda au vumbivumbi la ndani ya banda la kuku kwa sababu vumbi ni makazi mazuri ya Viroboto na Utitiri.

Lakini wakati mwingine unaweza kujitahidi kutumia dawa hizo za kunyunyiza kwenye mabanda na kuku wenyewe lakini zisifue dafu. Mara nyingi nimeliona hili kwenye mabanda mengi ya wafugaji. Sasa ukifikia katika hali hii ufumbuzi wa haraka ni kufanya usafi wa banda lako lote. Ondoa malanda na vumbi lote la samadi kisha deki kwa kutumia dawa ya V- RID Disinfectant. Pia utapaswa kupuliza dawa hiyo katika kuta za banda lako. Ukiona tabu kufanya hivyo basi baada ya kuondolewa samadi yote katika banda lako la kuku na kufuta vumbi kutani, deki kwa maji vuzuri bila dawa kisha baada ya banda kukauka vyema paka chokaa kote sakafuni kutani hadi dalini kama banda lako lina dali na kama halina basi utaishia tu katika kuta za banda na sakafuni.

Baada ya kukamilisha zoezi hilo ogesha kuku wako wote kwa kutumia dawa ya Paranex iliyochanganywa kwenye maji yaliyowekwa kwenye dishi kubwa la lita ishirini au arobaini au hata ndoo unaweza kitumia. Uogeshaji utafanyika kwa namna ya kumtumbukiza kuku mmoja mmoja katika lile dishi au ndoo kisha utamtoa. Ni tendo linalotumia chini ya nusu dakika. Unamtumbikiza unamtoa unamtumbikiza tena unamtoa ni kama mara mbili hivi lengo ni kuhakikisha kuwa dawa inapenya vizuri katika kila sehemu ya mwili wake.

Baada ya kukamilisha zoezi hilo basi kuku wako watarudi bandani wakiwa wako vizuri na visumbufu vyote vikiwa vimetokomezwa kabisa. Kutokea hapo utaanza kuona sasa afya ya kuku wako ikianza kuimarika na kama walikuwa walishaanza kutaga watarudi katika utagaji wao wa kawaida.

Angalizo. Unapotumia dawa ya kuogesha ni vizuri zoezi hili likafanyika mchana wakati jua linawaka ili kusudi kuku waweze kukingwa na athari ya baridi itakayowasababishia kupata nimonia. Vilevile ni vizuri ukawa na mtaalamu karibu atakayekusaidia kuchanganya dawa kwa uwiano sahihi na maji ili kuepusha madhara kama dawa haitachanganywa katika uwiano.

Aman Ng'oma
Mkurugenza Mtendaji
Kinasoru East Africa (T) Ltd
0767989713
Nduka street, Chamwino Bananza
Dodoma - Tanzania

Je, Una Habari,Picha,Tangazo,Makala, Ushauri n.k.?Basi Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp 0759 406 070

Post a Comment

 
Top