Shirika la Ariel Glaser Pediatric Aids Healthcare Initiative (AGPAHI) linalojihusisha na mapambano dhidi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) na Ukimwi nchini Tanzania limeendesha Kampeni ya Upimaji wa Maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi kwa watoto na vijana katika halmashauri ya Msalala na Manispaa ya Shinyanga katika mkoa wa Shinyanga.
Zoezi la kupima watoto na vijana limefanyika Juni 30,2017 na Julai 1,2017 katika zanahati ya Buluma iliyopo katika kijiji cha Buluma kata ya Jana katika halmashauri ya Msalala na zanahati ya kijiji cha Galamba katika kata ya Kolandoto katika manispaa ya Shinyanga.
Zaidi ya watoto na vijana 760 walipata fursa ya kupima afya zao.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo la upimaji,Afisa Mradi, Huduma Unganishi kwa Jamii AGPAHI mkoa wa Shinyanga, Charles Simon, alisema kampeni ya Upimaji VVU kwa vijana na watoto yenye kauli mbiu ya “Ijue Afya ya Mwanao” inalenga kuwafikia vijana na watoto wengi zaidi ili kujua afya zao.
“Hili ni zoezi endelevu,AGPAHI kwa kushirikiana na serikali tumekuwa tukipima afya za watoto na vijana na pale inapobainika wamepata maambukizi ya VVU huwa tunawaanzishia huduma ya tiba na matunzo”,alieleza Simon.
“Kupitia kampeni hii tunashirikiana na viongozi wa serikali za mitaa, vijiji na tumekuwa tukiwahamasisha wazazi kuwaleta watoto na vijana ili wapimwe na zoezi hili limekuwa na manufaa makubwa kwani watoto wengi wameletwa na wazazi wao kupima afya zao”,aliongeza.
Naye Mratibu wa Masuala ya Watoto AGPAHI mkoa wa Shinyanga,Dk. Jane Kashumba alisema wameamua kuanzisha kampeni hiyo ili kuwarahisishia wananchi kupata huduma ya kupima VVU kwa hiari katika maeneo ya karibu yao ili waweze kujua afya zao.
“Tunaushukuru mfuko wa kusaidia Watoto wenye VVU Kwa hisani ya watu wa Uingereza (CIFF) kwa kuwezesha kampeni hii",alieleza Dk. Kashumba.
"Tumeanza zoezi hili katika halmashauri hizi mbili na tutaendelea na kampeni katika maeneo mengine kwani lengo la AGPAHI ni kuwafikia watoto na vijana zaidi”,aliongeza Dk. Kashumba.
Kwa Upande wake Mratibu wa Wahudumu wa afya ngazi ya Jamii na Upimaji VVU wilaya ya Kahama, Peter Shimba alisema serikali itaendelea kushirikiana na shirika la AGPAHI katika mapambano dhidi ya VVU na Ukimwi.
Shirika la AGPAHI linatekeleza shughuli zake katika mikoa ya Shinyanga,Simiyu,Mwanza,Tanga,Geita na Mara kwa ufadhili wa Watu wa Marekani kupitia shirika la Centres for Disease Control and Preventation (CDC),mfuko wa kusaidia Watoto wenye VVU Kwa hisani ya watu wa Uingereza (CIFF) na Shirika la Development Aid From People to People (ADPP - Mozambique).
ANGALIA PICHA ZA MATUKIO WAKATI WA ZOEZI LA UPIMAJI WATOTO NA VIJANA KATIKA KIJIJI CHA BULUMA NA GALAMBA
Ijumaa Juni 30,2017: Hapa ni katika Zahanati ya Buluma iliyopo katika kijiji cha Buluma kata ya Jana halmashauri ya wilaya ya Msalala mkoa wa Shinyanga .
Afisa Mradi, Huduma Unganishi kwa Jamii AGPAHI mkoa wa Shinyanga, Charles Simon akiwaeleza wazazi na walezi walioleta watoto na vijana katika zahanati ya Buluma kuhusu lengo la Kampeni ya Upimaji wa Maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi kwa Watoto na Vijana.
Wazazi,vijana na watoto wakimsikiliza Afisa Mradi, Huduma Unganishi kwa Jamii AGPAHI mkoa wa Shinyanga, Charles Simonwakati akitolea ufafanuzi juu ya kampeni ya Upimaji VVU.
Mwenyekiti wa kijiji cha Buluma, Budila Teremka akisisitiza jambo kabla ya zoezi la kupima watoto na vijana halijaanza.
Mratibu wa Wahudumu wa afya ngazi ya Jamii na Upimaji VVU wilaya ya Kahama, Peter Shimba akizungumza kabla ya zoezi la upimaji VVU halijaanza ambapo alilishukuru shirika la AGPAHI katika harakati zake za mapambano dhidi ya VVU na Ukimwi na kwamba serikali itaendelea kushirikiana nalo katika mapambano hayo.
Mtoa huduma za afya akimtoa damu mtoto ili kumpima kama ana maambukizi ya VVU au la!
Kulia ni mzazi aliyeambatana na watoto wake katika zahanati ya Buluma kwa ajili ya kupima VVU.
Kushoto ni mama aliyekuwa ameambatana na watoto akishuhudia zoezi la upimaji VVU kwa watoto.
Zoezi la upimaji VVU likiendelea.
Mbali na kupima VVU, kulifanyika michezo ya watoto na vijana kama vile kukimbia na yai.Pichani kulia ni Charles Simon akitoa maelekezo kwa washiriki wa shindano la kukimbia na mayai.
Vijana wakikimbia na mayai yaliyowekwa kwenye vijiko.
Mchezo wa kukimbia na mayai ukiendelea.
Mratibu wa Wahudumu wa afya ngazi ya Jamii na Upimaji VVU wilaya ya Kahama,Peter Shimba akiipongeza moja ya familia iliyojitokeza kupima VVU na kubainika kuwa hawana maambukizi ya VVU. Katika zahanati ya Buluma kati ya watoto na vijana 525 waliopimwa VVU,watano pekee walibainika kuwa na maambukizi ya VVU.
Jumamosi Julai 1,2017: Hapa ni katika Zahanati ya Kijiji cha Galamba iliyopo katika kata ya Kolandoto manispaa ya Shinyanga ambapo pia Kampeni ya Upimaji wa Maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi kwa watoto na vijana imefanyika.
Mratibu wa Masuala ya Watoto AGPAHI mkoa wa Shinyanga,Dk. Jane Kashumba akizungumza wakati wa zoezi la kupima VVU kwa vijana na watoto katika kijiji cha Galamba.
Dk. Kashumba akizungumza na wazazi,vijana na watoto katika zahanati ya Galamba.
Mtoa huduma za afya akimchukua damu mmoja wa vijana kutoka kijiji cha Galamba waliofika kupima VVU.
Vijana na watoto wakisubiri kupima VVU.
Afisa Mradi, Huduma Unganishi kwa Jamii AGPAHI mkoa wa Shinyanga, Rehema Kivuyo akizungumza katika zahanati ya Galamba ambapo vijana na watoto 238 VVU na hakuna aliyepatikana kuwa na maambukizi ya VVU.
Michezo nayo ilikuwepo: Pichani ni Mratibu wa Masuala ya Watoto AGPAHI mkoa wa Shinyanga,Dk. Jane Kashumba akiongoza vijana katika mchezo wa kukaa kwenye viti.
Mchezo wa kukimbia na mayai ukiendelea.
Rehema Kivuyo akiwapa zawadi ya mayai vijana walioshinda mchezo wa kukimbia na mayai.
Vijana na watoto wakicheza mchezo wa kukimbiza kuku.
Picha zote na Kadama Malunde-Malunde1 blog
Post a Comment