Naibu
Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga (katikati) akioneshwa
ramani ya Hifadhi ya Taifa ya Saadani na Mwakilishi wa Mkuu wa Hifadhi
za Taifa, Vitalis Kuluka huku akishirikiana kuonesha eneo hilo na Katibu
Tawala wa Wilaya ya Bagamoyo,Erica Yigella ( wa pili kulia) mahali
kilipo Kitongoji cha Uvinje ambapo wakazi wa eneo hilo wamegoma kuhama
ndani ya hifadhi hiyo na wakati Naibu Waziri huyo alipotembelea hifadhi
hiyo jana. Wa kwanza kulia ni Afisa Wanyamapori, Godfrey Maro na Wa
kwanza kushoto ni Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Saadani, Stephano Msumi na
pande wa kulia nyuma ya Katibu Tawala ni Msaidizi wa Mkurugenzi Mkuu wa
Hifadhi za Taifa, Fredrick Mofulu
Naibu
Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga ( wa pili kulia )
akizungumza na Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Saadani , Stephano Msumi (
katikati) wakati Naibu Waziri huyo alipotembelea hifadhi hiyo jana kwa
ajili ya kujionea changamoto mbalimbali zinazoikabili . Wa kwanza kulia
ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Bagamoyo, Erica Yigella, Wa kwanza kushoto
ni Mwakilishi wa Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Vitalis Kuluka, wa tatu
kushoto ni Msaidizi wa Mkurugenzi Mkuu wa Hifadhi za Taifa, Fredrick
Mofulu
Naibu
Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga akizungumza jana na
Wananchi wa Kitongoji cha Uvinje ambao wamegoma kuhama ndani ya hifadhi
hiyo, wakati Naibu Waziri huyo alipotembelea kwa ajili ya kuzungumza nao
ili kujua ukubwa tatizo la mgogoro huo uliodumu kwa zaidi ya miaka 10
sasa .
Bango
lililopo katika geti la Gama linalokuelekeza sheria na taratibu ukiwa
unaingia katika Hifadhi ya Taifa ya Saadani iliyopo wilayani Bagamoyo
mkoani Pwani.
Naibu
Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga ( kushoto ) akipatiwa
maelezo na Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Saadani , Stephano Msumi (
katikati) wakati Naibu Waziri huyo alipotembelea hifadhi hiyo jana kwa
ajili ya kujionea changamoto mbalimbali zinazoikabili .Wa kwanza kulia
ni Mwakilishi wa Mkuu wa Hifadhi ya Taifa, Vitalis Kuluka, nyuma ya
Mhifadhi wa Saadani ni Msaidizi wa Mkurugenzi Mkuu wa Hifadhi za Taifa,
Fredrick Mofulu
Naibu
Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga ( mbele ) akiwa na baadhi
ya viongozi wa Hifadhi za Taifa pamoja kamati ya ulinzi na usalama
kutoka Wilayani Bagamoyo akiongoza kwenda kuangalia sehemu kunakofanyika
utalii wa boti katika Hifadhi ya Taifa ya Saadani wakati Naibu Waziri
huyo alipotembelea hifadhi hiyo jana kwa ajili ya kujionea changamoto
mbalimbali zinazoikabili .
Naibu
Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga (wa pili kulia) akipatiwa
maelezo na Msaidizi wa Mkurugenzi Mkuu wa Hifadhi za Taifa, Fredrick
Mofulu ( wali kushoto) kuhusiana na sehemu kunakofanyika utalii wa boti
katika Hifadhi ya Taifa ya Saadani . Wengine ni baadhi ya viongozi wa
Hifadhi za Taifa pamoja na kamati ya ulinzi kutoka Wilayani Bagamoyo .
Picha na Lusungu Helela
Wananchi
wa Kitongoji cha Uvinje kilichomo ndani Hifadhi ya Taifa ya Saadani
iliyopo wilayani Bagamoyo Mkoani wa Pwani wamesema hawapo tayari kuhama
wala kulipwa fidia ili kupisha hifadhi hiyo.
Kitongoji
hicho, ambacho ni kati ya vitongoji nane vya Kijiji cha Saadani,
kilitakiwa kiondolewe tangu mwaka 2005 baada ya hifadhi hiyo kupandishwa
daraja kutoka pori la akiba na kuwa hifadhi kwa mujibu wa Tangazo la
Serikali Namba 281 la Septemba 16, 2005.
Akizungumza
mbele ya kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya ya Bagamoyo, Naibu
Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga wakati alipofanya ziara
jana katika kijiji hicho aliwambia wananchi hao kuwa lengo la ziara yake
ni kutaka kuwasikiliza juu mgogoro huo na sio kuwahamisha.
‘Mimi
ni mgeni kidogo kwenye Wizara hii, Nimekuja kuangalia sio kuwahamisha
kwa kuwa sijui eneo hili lina ukubwa kiasi na lina kaya ngapi lakini
nimekuja kutembelea hifadhi na maeneo yote yenye changamoto. ‘’ alisema.Alisema
amefika kwa ajili ya kuwasikiliza ili aweze kujua jinsi mgogoro ulivyo
kwa sababu hakutaka kusikia upande mmoja wa TANAPA pekee.
Naye ,
Kaimu Mwenyekiti wa Kitongoji hicho, Hassan Akida alisema wakazi wa
eneo hilo hawapo tayari kuhama na wala kulipwa fidia kwa vile ni ardhi
yao tokea enzi za mababu zao.’‘Tumesema hapa ndo kwetu mnataka kutuhamisha mtupeleke wapi wakati sisi tumezoea maisha yetu hapa’’ alisema Akida.
Aliongeza
kuwa kitongoji hicho kimekuwapo kwa muda mrefu na waliishi bila shida
hadi pale pori hilo lilipobadilishwa na kuwa Hifadhi ya Taifa.“Wakati
hili ni pori la akiba tuliishi vizuri tu na wazazi wetu walikuwa ni
wafanyakazi wa pori. Lakini tangu iwe hifadhi imekuwa taabu. Sasa
tunafukuzwa wakati tumezaliwa hapa na wazazi wetu wamezikwa hapa hapa,”
anasema Hassan Akida.
Kwa
upande wa Mwenyekiti wa Kijiji cha Saadani, Adam Mwandosi alisema
mgogoro huo umedumu kwa muda mrefu na umekuwa ukileta chuki kati ya
Serikali na wananchi.Amesema
wananchi wa eneo hilo muda mwingine wamekuwa wakimuona hata yeye
Mwenyekiti wao kama anawasaliti kwa vile tokea mgogoro huo ulipoanza
viongozi wengi wamekuwa wakifika hapo lakini wamekuwa hawana majibu ya
kumaliza mgogoro huo.
Mhifadhi Mkuu wa Saadani, Stepahano Msumi amesisitiza kuwa kitongoji hicho kimo ndani ya hifadhi kinyume cha sheria.Alisisitiza kuwa sheria za hifadhi za Taifa haziruhusu makazi ya watu ndani yake.
“Kwa
ufupi tu ukiangalia GN (Tangazo la Serikali) linaonyesha kuwa eneo lote
la kitongoji cha Uvinje liko ndani ya hifadhi. Ni kweli lilikuwa eneo la
watu ambao walikuwa watumishi wa pori la akiba tangu lilipoanzishwa
mwaka 1968. Waliombwa kuondoka lakini waliendelea kuongezeka,” anasema.
Anasema
katika makubaliano, iliamuliwa kuwa walipwe fidia kwa taratibu lakini
hata hivyo licha ya kutekeleza utaratibu wa fidia bado wamegoma kuipokea
mbali ya wachache kujitokeza.
Ikumbukwe
kuwa, Saadani ni hifadhi pekee ya Taifa nchini na Afrika Mashariki
yenye fukwe za bahari na inayotazamana na Bahari ya Hindi na fukwe zake
zinakutana na uoto wa asili wa nchi kavu.
Inapatikana
katika mikoa ya Tanga na Pwani. Uwepo wake ni matokeo ya pori la akiba
la Saadani, ranchi ya Mkwaja na sehemu ya kaskazini, sambamba na akiba
ya msitu wa asili wa Zaraninge.
Post a Comment