Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akitoa
maelekezo kwa Kaimu Mtendaji Mkuu wa Kampuni Hodhi ya Rasilimali ya Reli
(RAHCO), Masanja Kadogosa (kushoto), kuhusu kusimamia kwa karibu mradi
wa ujenzi wa Reli ya Kisasa (Standard Gauge), wakati akikagua maendeleo
ya ujenzi wa mradi huo katika kijiji cha Soga Mkoani Pwani na Ngerengere
mkoani Morogoro.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (kushoto),
akimsikiliza Kaimu Mtendaji Mkuu wa Kampuni Hodhi ya Rasilimali ya Reli
(RAHCO), Masanja Kadogosa (kulia), alipomweleza hatua za ujenzi wa mradi
wa Reli ya Kisasa (Standard Gauge), wakati Waziri huyo alipokagua
maendeleo ya ujenzi wa mradi huo Mkoani Pwani.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa,
akichanganya zege katika moja ya Makalvati yanayojengwa katika mradi wa
Reli ya Kisasa (Standard Gauge), katika eneo la Kisarawe alipokagua
maendeleo ya ujenzi wa mradi huo Mkoani Pwani.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (katikati),
akibonyeza kitufe cha kuruhusu zege kwenda kwenye kalvati linalojengwa
kwenye Reli ya Kisasa (Standard Gauge), wakati alipokagua maendeleo ya
ujenzi wa mradi huo Mkoani Pwani.
Muonekano
wa moja ya kalvati linalojengwa kwenye Reli ya Kisasa (Standard Gauge),
katika eneo la Kisarawe Mkoani Pwani. Mradi huo unajengwa kwa awamu
mbili ambapo sehemu ya kwanza inajengwa kutoka Dar es Salaaam mpaka
Morogoro ambapo sehemu ya pili itajengwa kutokea Morogoro hadi
Makutupora mkoani Dodoma.
Mafundi
wa Kampuni ya Yapi Merkezi wakiendelea na kazi ya kujaza zege kwenye
moja ya kalvati linalojengwa kwenye Reli ya Kisasa (Standard Gauge),
katika eneo la Kisarawe Mkoani Pwani.
Tingatinga
likiendelea na kazi ya kuchenjua tabaka la chini la Reli ya Kisasa
(Standard Gauge), katika eneo la Soga, Mkoani Pwani.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa ametoa wito
kwa mkandarasi Yapi Merkezi na Motaengil Africa wanaojenga reli ya
kisasa (Standard Gauge Railway), kufanya kazi kwa uadilifu, kulingana na
vipimo vilivyo kwenye mkataba ili kuwezesha mradi huo kukamilika kwa
wakati.
Aidha,
ameitaka Kampuni Hodhi ya Rasilimali za reli (RAHCO), kuhakikisha kuwa
inafuatilia kwa karibu utekelezaji wa mradi huo kwani wananchi wamekuwa
wakisubiri kukamilika kwake na kuanza kupata huduma za usafiri wa treni
zitakazorahisisha shughuli zao za kibiashara na kijamii.
Akizungumza
leo mara baada ya kukagua mradi huo katika kijiji cha Soga mkoani
Pwani, Waziri Mbarawa amesema kuwa ameridhishwa na kasi ya wakandarasi
hao na kuagiza kuongeza spidi zaidi ili ifikapo mwaka 2020 mradi huo uwe
umekamilika.“Kasi mnayoenda nayo sio mbaya, ila naomba RAHCO
mhakikishe mnasimamia kwa karibu kuhakikisha spidi inaongezwa ili kazi
ikamilishwe haraka na kwa viwango”, amesema Profesa Mbarawa.
Akiwa
katika kijiji hicho, Waziri Mbarawa amemwagiza Kaimu Mtendaji Mkuu wa
RAHCO, Masanja Kadogosa, kukutana na uongozi wa kampuni hizo kujadili na
kuangalia fursa za upatikanaji wa ajira kwa watanzania hususan wakazi
wa eneo inapopita reli hiyo.
Kwa
upande wake, Kaimu Mtendaji Mkuu wa RAHCO, Masanja Kadogosa, amesema
mpaka sasa mradi huo upo ndani ya muda na kumhakikishia Waziri Mbarawa
kuwa mradi utakamilka kwa wakati kwani kazi inayofanyika sasa ni kuweka
zege kwa ajili ya ujenzi wa boksi kalvati ambapo kazi hiyo inaendelea
vizuri.
Ameongeza
kuwa katika kipindi hiki mradi ulisuasua kutokana na changamoto za mvua
za vuli, hivyo amefafanua kuwa wana mpango wa kuongeza kambi nyengine
nane upande wa Soga na nane upande wa Ngerengere ili kuhakikisha mradi
unakamilika kwa wakati.
Mradi
wa SGR unatekelezwa kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza unahusisha
ujenzi wa reli kutoka Dar es salaam – Morogoro na ya pili itahusisha
sehemu ya Morogoro hadi Makutupora mkoani Dodoma pamoja na njia za
kupishana ambapo kwa pamoja itakuwa na urefu wa kilometa 722 na
itajengwa kwa gharama ya shilingi Trilioni 7.1.
Post a Comment