Katibu
Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Dkt. Mpoki
Ulisubisya akisisitiza jambo kwa wataalamu wa sekta ya afya wakati wa
kongamano la ubunifu na utekelezaji wa huduma za tiba mtandao Tanzania
lililofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa LAPF, Dodoma.
Mtendaji
Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) Eng. Peter Ulanga,
akiwasilisha mada kuhusu umuhimu wa tiba mtandao nchini kwa wataalamu wa
sekta ya afya (hawapo pichani) wakati wa kongamano la ubunifu na
utekelezaji wa huduma za tiba mtandao Tanzania ambalo limeandaliwa na
UCSAF lililofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa LAPF, Dodoma.
Kaimu
Mkurugenzi wa TEHAMA, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Eng.
Peter Phillip Mwasalyanda (aliyeketi katikati), akisikiliza kwa makini
kongamano la ubunifu na utekelezaji wa huduma za tiba mtandao Tanzania
ambalo limeandaliwa na UCSAF lililofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa
LAPF, Dodoma
Wataalamu
wa sekta ya afya wakifuatilia kwa makini maelekezo ya Katibu Mkuu wa
Wizara ya Afya, Dkt. Mpoki Ulisubisya (hayupo pichani) wakati wa
kongamano la ubunifu na utekelezaji wa huduma za tiba mtandao Tanzania
ambalo limeandaliwa na UCSAF lililofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa
LAPF, Dodoma
Serikali
imejipanga kutumia tiba mtandao kuboresha huduma za afya nchini kwenye
hospitali zote za ngazi ya taifa, rufaa na wilaya ili kuwawezesha
wagonjwa waishio sehemu mbali mbali nchini kupata huduma za afya kwa
wakati na kwa ufanisi.
Hayo
yameelezwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto, Dkt. Mpoki Ulisubisya wakati akifungua kongamano la
ubunifu na utekelezaji wa huduma za tiba mtandao Tanzania lililofanyika
kwenye ukumbi wa mikutano wa jengo la LAPF, Dodoma.
Dkt.
Ulisubisya amesema kuwa lengo la kongamano hilo ni kuwakutanisha
watendaji wakuu wa hospitali za taifa nchini, madaktari bingwa wa sekta
ya Afya, wakuu wa taasisi zinazoshughulika na sekta ya Afya, Wizara ya
TAMISEMI, Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano; taasisi nyingine za Serikali;
sekta binafsi na wabia wa maendeleo ili kujadiliana na kuwa na uelewa
wa pamoja wa kufanikisha utekelezaji wa huduma za tiba mtandao ili
kuboresha huduma za afya nchini.
Amesema
kuwa tiba mtandao itawezesha na kuongeza ufanisi katika kufanya
uchunguzi, utoaji wa tiba na madawa kwa wagonjwa wanaosumbuliwa na
magonjwa mbalimbali yasiyoambukiza na yanayotokana na ajali za
barabarani. “Hadi hivi sasa ni asilimia 37 tu ya wagonjwa wa kifua kikuu
ndio wanaotambulika na kupatiwa huduma na Wizara ya Afya katika
hospitali mbalimbali nchini. Hivyo, tiba mtandao itawezesha upatikanaji
wa wagonjwa na ufikishaji wa huduma kwao kwa wagonjwa wengine asilimia
63”, amefafanua Dkt. Ulisubisya.
Ameongeza
kuwa tiba mtandao itapunguza gharama za wagonjwa na wanaowahudumia
kusafiri kufuata madaktari. Aidha, amewataka wakuu hao wa taasisi
kuwaruhusu wataalamu wao, wa Wizara ya TAMISEMI na wa Wizara ya Afya,
kushiriki mafunzo ya tiba mtandao ili kuongeza ufanisi wao katika
kuhudumia wagonjwa.
Amewataka
wataalamu wa afya na wakuu wa taasisi zinazohusika na masuala ya afya
kununua vifaa tiba vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA)
vyenye viwango na ubora unaohitajika ili kuwezesha tiba mtandao na
manunuzi hayo yazingatie na kufuata ununuzi wa pamoja wa huduma na
bidhaa za Serikali.
Vifaa
vya kisasa vya TEHAMA vinavyohusika na tiba mtandao vitawawezesha
wataalamu kufanya uchunguzi kwa mgonjwa, kupata majibu ya uhakika na
kumpatia mgonjwa tiba inayostahili na ya uhakika. Aidha, amemuelekeza
Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Eng. Ulanga,
ambao ndio waanadaji na waratibu wa kongamano hilo, kushirikiana na TTCL
kuhakikisha kuwa tiba mtandao inapatikana katika hospitali zote za
rufaa na hospitali ambazo zina changamoto ya kijiografia ya kufikika kwa
urahisi. Aidha, hadi hivi sasa huduma ya tiba mtandao inapatikana
katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Bagamoyo, KCMC-Moshi,
Bugando-Mwanza na Benjamin Mkapa, Dodoma.
Naye
Eng. Ulanga amesema kuwa UCSAF imeanzisha huduma ya tiba mtandao kwenye
vituo 14 vya majaribio. Aidha, imeainisha orodha ya vituo 279 ikiwa ni
pamoja na hospitali za taifa, rufaa na wilaya ambazo zitaunganishwa na
kuwezeshwa kutoa huduma ya tiba mtandao nchini.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Hospitali ya Saratani ya Ocean Road, Dar es Salaam Dkt.
Julius Mwaiselage, akiwa mmoja wa washiriki wa kongamano hilo amesema
kuwa, tayari tulikuwa tunatumia huduma ya tiba mtandao kwa wagonjwa wetu
kwa kushirikiana na hospitali nyingine zilizopo nchini India kwa
kuwafanyia wagonjwa uchunguzi na kuona kama kweli mgonjwa husika
anahitaji kupelekwa nje ya nchi kwa matibabu zaidi.
“Uwepo
wa huduma ya tiba mtandao kwenye hospitali zetu nchini, itatuwezesha
kufanya uchunguzi na kutoa tiba kwa wagonjwa waliopo mikoani hivyo
kuwapunguzia gharama wagonjwa za kuja Dar es Salaam na endapo
watalazimika kuja basi watakaa kwa muda mfupi ukilinganisha na hapo
awali”, amesema Dkt. Mwaiselage. Washiriki wengine wa kongamano hilo ni
kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Bugando, MOI, Taasisi ya Moyo ya
Jakaya Kiwete, Mloganzila, Aga Khan, Hospitali ya Rufaa Mbeya, NHIF,
PATH na Shirika la Afya Duniani.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano







Post a Comment