Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Baadhi ya wanafunzi wakiwa na walimu wao wakijaribu kupata ufafanuzi toka kwa uongozi wa chuo hicho.

Mazungumzo yakiendelea ndani ya ukumbi na uongozi wa chuo hicho 


Picha na Davd Nyembe wa Fahari News

Na Mwandishi wetu,Mbeya
WANAFUNZI wa Chuo cha Ufundi cha Kanisa la Moravian, Jimbo la Kusini Magharibi, wamegoma na kutishia kukatisha masomo yao kwa kile wanachokidai kuchoshwa na kauli za fedheha na matusi zinazotolewa na

Mkuu wao wa chuo  hasa pale  wanapodai haki zao za msingi.
Tuhuma hizo ambazo ziliambatana na vurugu za kutishia kuzivunja ofisi za chuo hicho huku baadhi yao wakilizunguka eneo hilo, wakimsubili Mkuu wa chuo hicho, God Lwinga kutoka nje kwa madai ya kumshushia kipondo.

Vurugu hizo zilianza majira ya asubuhi, ambapo wanachuo hao, wapatao 83 wa  kozi za umeme, ushonaji na ufundi selemala, walilizingira eneo la geti  kwa lengo la kuzuia gari la kiongozi huyo, ili asitoke nje kisha kutimiza lengo lao.

Wakati, wanachuo hao wakiendelea na jaribio hilo, inasemekana Mkuu huyo wa chuo alitoa taarifa polisi ya kuomba msaada, ambapo askari polisi walifika na kufanikiwa kutuliza  vurugu hizo ikiwa na kunusuru kichapo alichokusudiwa kupewa  kiongozi huyo.
Wakizungumza  kwenye mkutano wa makubaliano ulioitishwa na na uongozi wa chuo hicho kwa kushirikisha viongozi wa jeshi la polisi, Wanafunzi hao, walisema kuwa  Mwalimu Mkuu huyo, amejenga tabia ya kuwadharau  kwa kutoa lugha za matusi na kejeli pale wanapofikisha matatizo yao.

Wamesema, Mwaka jana, uongozi wa chuo uliwasilisha mfumo upya wa ufundishaji wa masomo chuoni hapo kutokana na uongozi wa Veta kutoa mtaala mpya wa kufundishia ambao umeweka bayana kwamba wanafunzi watahitajika kusoma miaka mitatu badala ya miwili  ili kupata cheti kinachotambulika na serikali.

Wamesema, hivyo wao kama walengwa amabao walitakiwa kumaliza elimu hiyo mwaka huu kabla ya mabadiliko hayo walimfuata kiongozi huyo kwa lengo la kuwasilisha maoni yao  kutokana na changamoto zinazowakabili, jambo ambalo limeonekana kuwa kero kwa Mkuu huyo wa chuo hivyo kudaiwa kutumia lugha hizo za matusi ambazo zimeonekana kuwakera wanafunzi hao.

Akijibu malalamiko hayo ya wanafunzi, Mkuu wa Chuo hicho, God Lwinga, alisema  yeye hakubaliani na tuhuma zinazotolewa na wanafunzi hao kwani uongozi wa chuo ulishawaeleza kila kitu na wao walikuwa wanaufahamu mkakati huo wa Veta.

Hata hivyo, Mkuu huyo aliwataka wanafunzi hao walio na utayari wa kuendelea na masomo kuandika barua na watakao ona elimu waliyoipata inawatosha basi wanaweza kuendelea na shughuli zao za kutafuta maisha kupitia ujunzi huo walioupata.

Mwisho.

Je, Una Habari,Picha,Tangazo,Makala, Ushauri n.k.?Basi Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp 0759 406 070

Post a Comment

 
Top