Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This
Na EmanuelMadafa,Mbeya
MKUU wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro, ameziagiza halmashauri zote mkoani Mbeya kuwachukulia hatua za kinidhamu watendaji watakabaoinika kuwa chanzo cha kuzalisha hoja za ukaguzi zitakazobainishwa na Mkaguzi na Mdhibiti wa fedha za Serikali (CAG).

Amesema hatua hiyo ni  kutokana na uzembe wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwenye idara zao.

Kandoro ametoa agizo hilo kwenye kikao Maalum cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Chunya kilichoandaliwa kwa ajili ya kupitia hoja za ukaguzi wa hesabu za fedha za halmashauri hiyo ambapo katika taarifa hiyo hoja 80 hazijapatiwa ufumbuzi.

Amesema kuwa ofisi yake haitavumilia tabia ya watendaji kuzalisha hoja kutokana na uzembe na hivyo ameagiza Mabaraza ya Madiwani kuanza kuchukua hatua dhidi ya watendaji hao na taarifa ya hatua hizo za kinidhamu itolewe kabla ya kufanyika vikao vya kupitia hoja za ukaguzi.

Amesema ikiwa hatua stahiki hazitachukuliwa dhidi ya watendaji hao, itabidi viongozi wenye dhamana ya kuwachukulia hatua na wao wawajibike kutokana na kulea uzembe kwenye maeneo yao.

Agizo hilo la Mkuu wa Mkoa lilitokana na Taarifa ya ukaguzi ya Halmashauri ya Wilaya ya Chunya kuonyesha kuwa  licha ya halmashauri hiyo kupata hati safi ya ukaguzi, lakini kulikuwepo na hati chafu katika mradi wa maji.

Amesema kuwa hati hiyo chafu kwenye mradi wa maji inaitia doa halmashauri hiyo, hivyo kuagiza watendaji wanaosababisha kuwepo kwa hati chafu kwenye idara yao washughulikiwe.

Hata hivyo Kandoro aliipongeza Halmashauri hiyo kwa kupata hati safi ya ukaguzi pamoja na kuongoza kwa makusanyo ya mapato ya ndani ikilinganishwa na Halmashauri zote mkoani Mbeya.
                  

mwisho      

Je, Una Habari,Picha,Tangazo,Makala, Ushauri n.k.?Basi Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp 0759 406 070

Post a Comment

 
Top