Na Boniface Wambura,Dar es salaam
Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF) imekutana leo (Septemba 7 mwaka huu) na kupitia masuala
mbalimbali ikiwemo mgogoro wa kimkataba kati ya klabu ya Yanga na mchezaji
Emmanuel Okwi.
Mkataba huo ulipitiwa na Kamati ikiwemo
kumsikiliza mchezaji mwenyewe pamoja na upande wa Yanga, na kuridhika kuwa
mkataba kati ya pande hizo umevunjika.
Ukiwa ni mkataba wa pande mbili, Yanga ilikiuka kipengele namba 8
kuhusu malipo ya ada ya usajili.
Yanga ikiwa mwajiri, haikutekeleza kipengele hicho cha kimkataba
hadi kufikia Juni 27 mwaka huu ilipoandika barua TFF kuomba mkataba huo
uvunjwe. Kwa maana hiyo Okwi ni mchezaji huru, hivyo yuko huru kujiunga na timu
yoyote.
Mkataba ni uhusiano kati ya mwajiri (Yanga) na mwajiriwa (Okwi),
ambapo Kamati imebaini kuwa uhusiano huo haupo, hivyo hakuna mazingira ya pande
hizo mbili kuendelea kufanya kazi pamoja.
Pamoja na Yanga kuwasilisha pingamizi la kuwepo mmoja wa wajumbe
katika kikao kwa sababu za kimaslahi (conflict of interests), walifahamishwa
kuwa kilichopo mbele ya kamati ni mgogoro wa kimkataba kati ya Yanga na Okwi,
na si usajili.
Pia lilijitokeza suala la Okwi kutakiwa na klabu ya Wadi Degla ya
Misri. Kamati imeiagiza Sekretarieti ya TFF kulifanyia uchunguzi suala hilo na
kulitolea taarifa katika kikao kijacho.
Hata hivyo mjumbe huyo hakushiriki katika kuchangia hoja na kutoa
maamuzi. Uamuzi wa kamati ulifanyika baada ya majadiliano, hivyo hakukuwa na
suala la kupiga kura.
Kuhusu pingamizi la Coastal Union kwa Abdi Banda, Kamati imebaini
kuwa klabu hiyo imevunja mkataba kati ya pande hizo mbili kwa kushindwa kumlipa
mchezaji huyo mshahara wa miezi mitatu mfululizo kama takwa la mkataba.
Klabu ya Coastal Union iliwakilishwa na mmoja wa viongozi wake,
wakati Banda aliwakilishwa na mwanasheria wake.
Vilevile Kamati imekubaliana na pingamizi
la Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Morogoro (MRFA) kuhusu wachezaji
waliofanyiwa uhamisho kutoka katika mkoa wake bila kulipiwa ada za usajili,
hivyo klabu husika zinatakiwa kulipa ada hizo.
Pia Kamati imeagiza klabu zote
zilizosajili wachezaji bila kuwafanyia uhamisho, kulipa ada za uhamisho kwa
pande husika kabla ya kuanza ligi, vinginevyo leseni zao zitazuiwa hadi
watakapolipa.
Mashauri mengine ya pingamizi
yatasikilizwa baadaye kwa vile klabu husika hazikupata fursa ya kufika mbele ya
kamati.
Kamati inasisitiza kwa wanachama wa TFF
kuheshimu mikataba.
Post a Comment