Na EmanuelMadafa,Mbeya
MKUU wa Wilaya ya Mbozi, Dk. Michael Kadege,
ametajwa kuwa ni miongoni mwa watendaji na viongozi wanaodaiwa kuhusika na
ubadhilifu wa fedha za umma wa shilingi Bilioni 1.
Ubadhilifu huo wa fedha hizo za serikali,
uliibuliwa kwenye taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti wa hesabu za serikali (CAG)
katika mwaka wa fedha wa 2013/14 ndani ya halmashauri hiyo.
Wakizungumza mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya,
Abbas Kandoro,
wakati wa kikao maalum cha Baraza la Madiwani
kilichokuwa kikipitia hoja za mkaguzi na mdhibiti wa hesabu za serikali(CAG)
baadhi ya madiwani hao, walisema Mkuu huyo wa Wilaya, amekuwa akitumia fedha za
halmashauri nje ya bajeti kwa matumizi yake binafsi.
Diwani huyo, aliendelea kueleza kuwa baadhi ya
nyaraka ambazo alidai kuwa nazo, zinaonyesha jinsi kiongozi huyo alivyokuwa
akitumia fedha hizo, ambapo Mwezi Agosti mwaka huu, nyaraka moja imeweka bayana
kwamba kiongozi huyo alikuwa akilipwa kiasi cha shilingi milioni 4 kila mwezi
kwa ajili ya kile kilichodaiwa ni safari za kuitwa Ikulu.
Hata hivyo, ndani ya ukumbi tuhuma hizo
zilipingwa na Diwani wa Kata ya Miyovizi, Cosmas Nzowa, akidai kuwa tuhuma
zilizotolewa na Diwani mwenzake ambao wote wanakiwakilisha chama cha mapinduzi
(CCM) kuwa ni majungu, na kwamba hana ushahidi wowote isipokuwa ni ubabaishaji
tu.
Kutokana na malumbano hayo, Mkuu wa Mkoa wa
Mbeya, Abbasi Kandoro, alionya dhidi ya hali hiyo kwa kuwataka madiwani na
viongozi wa serikali, kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa taratibu kwa kuwa
wote wapo hapo kwa ajili ya kuwatumikia wananchi, badala ya kujikita kwenye
misuguano ya makundi.
Hata hivyo, akihitimisha kikao hicho, Mwenyekiti
wa Halmashauri hiyo, Elick Ambakisye, alimuomba Mkuu wa mkoa kulifuatilia kwa
umakini suala hilo kwa kuwa hali ni mbaya na imefika mahala viongozi hao
wanawindana kama njiwa kwa kutaka kuuana.
Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi kwa miaka mitatu
mfululizo imekuwa ikipata hati yenye mashaka ye hesabu za ukaguzi, huku pia
ikishika nafasi ya mwisho kwa ukusanyaji wa mapato kati ya halmashauri 10 za
Mkoa wa Mbeya.
mwisho
Post a Comment