Mkuu wa Kitengo cha Usalama Tanesco Mkoa wa Mbeya Bw.Cyprian Lugazia akiwa katika moja ya majukumu yake ya kukamata wahujumu wa shirika hilo. |
Na EmanuelMadafa,
WANAWAKE wawili wanashikiliwa na Shirika la Umeme Tanzania
(Tanesco) Mkoa wa Mbeya, kwa tuhuma za kuhusika na uuzaji na usambazaji wa
mafuta ya Transfoma.
Wanawake hao, ambao ni wakazi wa eneo la Ilomba lililopo Jijini
Mbeya, walikamatwa jana majira ya saa mbili usiku, wakiwa na lita 10 za mafuta
hayo, wakitafuta wateja wa kuwauzia.
Kwa mjibu wa taarifa kutoka kwa Mkuu wa Kitengo cha Usalama cha
Tanesco Mkoa wa Mbeya,Cyprian Lugazia aliwataja wanawake hao kuwa ni Grace
Jeremia maharufu kwa jina la (Mama Matha) ambaye ni muuzaji mzoefu na Sera
Zakaria.
Aidha, Afisa huyo, amesema watuhumiwa hao walikutwa na madumu hayo
mawili ya lita tano kila moja na kuwa mpaka sasa maofisa wa shirika
hilo wanaendeleza msako mkali dhidi ya watu wengine ambao wamekuwa wakilihujumu
shirika hilo na kusababisha hasara kubwa kwa serikali.
“Watuhumiwa hawa watafikishwa mahakamani mara uchunguzi wa polisi
kwa kushirikiana na maofisa wa shirika utakapokamilika,”alisema.
Kwa upande wake Meneja wa Tanesco Mkoa wa Mbeya Mhandisi Amosi
Maganga, amesema mafanikio ya kukamatwa kwa watuhumia hao yametokana na
ushirikiano unaondelea baina ya shirika hilo na wananchi ambao wamekuwa wakitoa
taarifa za watu ambao wamekuwa wakilihujumu shirika kwa kujihusisha na vitendo
vya wizi wa mafuta pamoja na umeme.
Amesema, shirika limekuwa likiingia hasara kubwa katika upotevu wa
mafuta hayo ya Transfoma ambapo ndi chanzo kikubwa cha kusababisha kuungua kwa
transfoma hizo, hali inayochangia baadhi ya wanachi kushindwa kupata huduma
hiyo ya umeme.
“Ukiangalia katika kipindi cha miezi sita shirika limepata hasara
ya shilingi bilioni moja, hivyo ni vema wananchi wakaendelea kutoa ushirikiano
ili watu hawa wakamatwe na kuchukuliwa hatua za kisheria,”alisema.
Hata hivyo, ametoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa na
kuwa kwa yeyote atakayefanikisha kukamatwa kwa wahusika atapewa zawadi nono.
Mei 20 mwaka huu Tanesco Mkoa wa Mbeya, lilimkamata Mwantika
likimtuhumu kujiunganishia umeme kinyemela na majirani zake na tayari
amefikishwa mahakamani.
Mwisho.
Post a Comment