Mwenyekiti wa ccm Mbeya Godfrey Zambi |
Na Mwandishi wetu,Momba
Baadhi ya wafanyabiashara waliovunjiwa maduka yao katika Mji
mdogo wa Tunduma Wilayani Momba, wamesema wanakusudia kukiburuza
mahakamani Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Mbeya kwa madai ya kukiuka kwa mkataba
wao waliowekeana wakati wa upangishaji wa maduka hayo..
Wakizungumza na Blog hii,
wafanyabiashara hao wanaoendesha shughuli zao za kibiashara katika eneo la Mji
mdogo wa Tunduma, walidai kuwa, mkataba huo umevunjwa kiholela na
haukufuata taratibu waliokuwa wamekubaliana kati yao na uongozi wa chama hicho.
Walisema mapatano hayo yalifanyika mwezi wa
kwanza mwaka huu ambapo waliandikishiana mkataba wa miaka 10 na mmiliki huyo
ambaye ni chama cha mapinduzi na kwamba kila mwaka mfanyabiashara
atawajibika kukilipa chama kiasi cha shilingi 300,000 ikiwa kama pango la
chumba hicho.
Walisema kuwa mapatano hayo pia yalikuwa na masharti ambayo
yalimtaka mpangaji endapo atakatisha mkataba atatakiwa kutoa taarifa ya mwezi
mmoja huku mpangishaji atatakiwa kutoa taarifa ndani ya mwezi mmoja jambo
ambalo halijafanyika.
Akielezea sababbu iliyomfanya, kukusudia kukipeleka mahakamani,
chama hicho mfanyabiashara huyo, Anyegile Mwamalika, alisema licha ya makataba
huo kuvunjwa kiholela pia wahusika wanadaiwa kuondoka na bidhaa iliyokuwemo
ndani, thamani yake ikiwa ni zaidi ya milioni 40.
“Wakati tukio hili linatokea sikuwepo, lakini kijana wangu
alikuwepo ambaye ndiye alikuja kunieleza, nilipomuhoji ya kwamba endapo
wahusika hao walimuhalifu au kumuonyesha kibali chochote kilichotolewa na
mahakama, alinikatalia,”alisema mfanyabiashara huyo.
Alisema, tukio hilo linadaiwa kutekelezwa na Tume ya uchunguzi
iliyoundwa na CCM Mkoa wa Mbeya, kufika kuchunguza tuhuma mbalimbali za
ubadhilifu wa fedha unaodaiwa kufanywa na viongozi wa Kata hiyo ya Tunduma.
“Sitaki kwenda mbali lakini ninachodai ni haki yangu kwani mimi
sikuvamia kibanda hicho nilikipata kihalali, tayari nimezungumza na mwanasheria
wangu hivyo ninakusudia kulifikisha suala hili mahakamani kwani mpaka sasa
sifahamu mzigo wangu ulipohifadhiwa,”alisema.
Akizungumzia tatizo hilo kwa njia ya simu, mfanyabiashara mwingine
ambaye jina lake limehifadhiwa, alisema kitendo cha Tume hiyo kuvunja duka
lake, kimemuingizia hasara kubwa sana kwani mpaka sasa hajui mzigo wake
ulipohifadhiwa.
“Ninatarajia kuwasili Tunduma kesho, kwani nipo safarini Dar es
Salaam, habari ya kuvunjwa kwa duka langu nimeipata kwa njia ya simu tu hivyo
nitakapowasili hapo na kujihakikishia ndipo nitaamua ni hatua gani
nichukue,”alisema mfanyabiashara huyo.
Aidha, wafanyabiashara hao, wamekitilia mashaka kitendo hicho na
kukihusisha na vitendo vya rushwa au chuki binafsi kwani maduka yaliyovunjwa ni
machache na mengine yameachwa huku wamiliki wote waliingia mkataba kwa kipindi
kimoja.
Hata hivyo wameutaka uongozi huo wa Chama ngazi ya Mkoa, kutumia
busara na haki katika utatuzi wa suala hilo kwani kila mmoja amekuwa akitafuta
maisha na kusomesha watoto.
Akizungumza kwa njia ya simu, Msemaji wa Chama hicho, Katibu
Mwenezi wa CCM Mkoa wa Mbeya, Bashiru Madodi, alikiri kutokuwa na taarifa ya
uharibifu huo na kuhaidi kulifanyia kazi suala hilo.
“Taarifa hiyo ndio ninaipata kutoka kwako lakini nilichokuwa ninakifahamu
ni Tume kumaliza kazi tuliyowatuma ya kuchunguza tuhuma zinazowakabili viongozi
wa Kata ya Tunduma juu ya ubadhilifu wa milioni za fedha,”alisema Madodi.
Alisema, Chama kiliituma Tume kwenda kuchunguza tuhuma si
kutekeleza majukumu mengine hivyo endapo itabainika tume ilikiuka taratibu na
maagizo ya chama nayo itachukuliwa hatua za kinidhamu.
Hata hivyo, Madodi alikiri kwa Tume yake kukamilisha kazi
iliyotumwa na chama ya kuchunguza tuhuma zinazowakabili viongozi wa Kata ya
Tunduma Wilayani Momba, ambao ni Hemed Steven, Katibu, Boniface Mwakasega
Mwenezi, Zainabu Siame mchumi na Mwenyekiti Daniel Mwashuya hivyo baada ya hapo
chama kitapitia taarifa hiyo na kutolea maamuzi.
mwisho
Post a Comment