Na Boniface Wambura,Dar es salaam
Michuano ya Ligi Daraja la Pili (SDL) msimu huu iliyokuwa ianze
kutimua vumbi Novemba 22 mwaka huu kwa mechi kumi katika viwanja vitano tofauti
imesogezwa mbele hadi Desemba 6 mwaka huu.
Mechi hizo zimesogezwa ili kutoa fursa ya kukamilisha maandalizi
mbalimbali ya ligi hiyo inayoshirikisha timu 24 kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania
Bara.
Mikoa yenye timu katika ligi hiyo ni Arusha, Dar es Salaam,
Dodoma, Iringa, Katavi, Kigoma, Lindi, Mara, Mbeya, Morogoro, Mwanza, Njombe,
Pwani, Rukwa, Ruvuma, Shinyanga, Singida na Tabora.
Wakati huo huo Mashindano ya Taifa kwa vijana wenye umri chini ya miaka 12
yanayoshirikisha kombaini za mikoa yote ya Tanzania yatafanyika jijini Mwanza
kuanzia Desemba 30 mwaka huu hadi Januari 5 mwakani.
Awali mashindano hayo yalipangwa kuanza Desemba 6 mwaka huu,
lakini yamelazimika kuyasogeza ili kutoa fursa ya kukamilika kwa matengenezo ya
viwanja vitatu ambayo vitatumika.
Kila timu ya mkoa inatakiwa kuwa na ujumbe wa watu 16, wakiwemo
wachezaji 14 na makocha wawili katika mashindano hayo ya timu yenye wachezaji
saba (7 aside).
Timu zinatakiwa kuwasili jijini Mwanza kuanzia Desemba 28 mwaka
huu tayari kwa ajili ya uhakiki wa umri na taratibu nyingine za mashindano.
Timu zote zitafikia katika shule ya Alliance (Alliance Schools).
Wachezaji wanaotakiwa kushiriki mashindano hayo ni wenye umri
chini ya miaka 12, hivyo ni wale waliozaliwa kuanzia Januari 2003 na kuendelea.
Post a Comment