Waziri Mkuu mstaafu Joseph Warioba akisaidiwa kutolewa katika vurugu |
Mdahalo
huo uliokuwa ukitangazwa moja kwa moja kupitia redio na televisheni ulivurugika
kutokana na kundi la vijana wapatao 20 kuanza kumzomea aliyekuwa mwenyekiti wa
Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, alipokuwa akiwasilisha mada
yake.
Vijana
hao ambao haijajulikana walitokea wapi au walikuwa na ajenda gani waliinua
mabango ya kupinga msimamo wa waliokuwa wakiendesha mdahalo na kusema rasimu ya
katiba iliyopendekezwa inakidhi mahitaji yote na kusema hakuna haja ya mdahalo.
Jaji
Warioba ambaye ni Waziri Mkuu mstaafu wa Tanzania alifanikiwa kutoka nje ya
ukumbi ulipokuwa ukifanyika mdahalo huo mjini Dar Es Salaam, lakini wapo watu
waliojeruhiwa kutokana na kurushwa viti na vitu vingine.
BBC
iliwasiliana na Jaji Warioba apate kueleza yaliyotokea na kama yuko salama
baada ya vurugu hizo, lakini aliomba radhi kwa kusema hayupo tayari
kulizungumzia swala hilo.
Kiongozi
wa kitengo cha hamasa umoja wa vijana CCM (UVCCM), Paul Makonda, aliyekuwepo
ukumbini alidaiwa kuhusika na vurugu. Lakini alipoulizwa na BBC kujibu tuhuma
hizo Bw Makonda amekanusha kuhusika nazo huku akisema kwamba alihudhuria
mdahalo kwasababu ulikuwa wazi kwa kila mtu.
Wakati
wa vikao vya Bunge Maalum la Katiba mjini Dodoma, Makonda aliwahi kutoa kauli
za kumkebehi Jaji Warioba ambaye tume yake iliandaa rasimu ya iliyokuwa
ikijadiliwa na bunge hilo.
Hata
hivyo Kamanda wa Polisi mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura, aliieleza BBC
kuwa hana maelezo ya kutosha na kwamba atalizungumzia akipata taarifa rasmi ya
kiofisi.
Tanzania
ipo katika mchakato wa kupata katiba mpya. Rasimu iliyodaliwa na kupitishwa na
bunge lililosusiwa na vyama vya upinzani inatarajiwa kupigiwa kura na wananchi
mwezi Aprili, 2015.
Wachambuzi
wa maswala ya kisiasa wameeleza wasi wasi kuwa endapo hakutakuwa na kuvumiliana
hali ya kisiasa nchini humo inaweza kubadilika na kuleta ghasia ambazo zinaweza
kuepukika.CHANZO BBC
Post a Comment