Na Mwandishi wetu Mbeya
JESHI la Polisi Mkoani Mbeya, linawashikilia
madereva watatu wa mabasi ya abiria yanayofanya safari zake kati ya Mbeya na
Dar es salaam, baada ya kukutwa wakijiandaa kusafirisha abiria wakiwa wamelewa.
Katika sakata hilo, mabasi mengine matatu pia
yametozwa faini na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini
(Sumatra) kwa kosa la kutokuwa na madereva wawili pamoja na vibali vya
kusafirisha abiria.
Watuhumiwa hao walikamatwa jana wakati Jeshi
hilo na Sumatra walipofanya ukaguzi wa kushtukiza kwenye Kituo Kikuu cha Mabasi
cha Jijini Mbeya.
Akizungumza wakati wa ukaguzi huo, Kamanda wa
Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Mbeya, Butusyo Mbwambelo alisema kuwa
madereva hao wamekamatwa baada ya kupimwa na kukutwa na viwango mbalimbali vya
ulevi.
Alisema Madareva wawili kati yao ni wa Kampuni
ya Nganga na dereva mmoja ni wa kampuni ya Alhushoom ambayo yanafanya safari
zake kati ya Mbeya na Dar es Salaam.
Amesema, kwa kawaida dereva hapaswi kuzidisha
kiwango cha ulevi cha mg 0.8, lakini madereva hao walikuwa na kiwango cha juu
cha ulevi cha mg 13.0, 118.0 na mg 123.0.
Amesema kuwa dereva mwingine baada ya kupimwa na
kubainika kuwa amelewa alikimbia na hivyo Jeshi la Polisi linaendelea kumtafuta
ili sheria iweze kuchukua mkondo wake na kwamba madereva waliokamatwa
watafikishwa mahakamani.
Kwa upande wake Afisa Mfawidhi Sumatra mkoani
Mbeya, Denis David amebainisha kuwa katika ukaguzi wake, alibaini kuwepo kwa mabasi
matatu yanayosafiri umbali mrefu ambayo hayakuwa na madereva wawili kama
ambavyo masharti ya leseni yanavyoelekeza.
Amesema kuwa mabasi hayo yametozwa faini ya
shilingi 250,000 kila moja na kutakiwa kutafuta dereva wa pili kabla ya kuanza
safari.
Mwisho.







Post a Comment