Na Boniface Wambura,Dar es Salaam
Mechi ya Nani Mtani Jembe 2 kati ya Simba na Yanga zinazodhaminiwa
na Kilimanjaro Premium Lager itachezwa Jumamosi, Disemba 13, 2014 saa kumi
kamili jioni kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Akizungumza
na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Meneja Udhamini wa TBL, George
Kavishe amesema kwamba “Tayari Simba na Yanga zimesaini makubaliano ya kucheza
mechi ya Nani Mtani Jembe 2 (Nani Mtani Jembe 2 Match).
Pambano hili ni zawadi
ya kufungia mwaka kwa mashabiki na kila timu imetia saini makubaliano kwamba
itachezesha kikosi cha kwanza ili kuwapa mashabiki burudani ya uhakika.”
Kavishe
aliongeza kuwa mechi hii ni maalumu kwa ajili ya kuhitimisha kampeni ya Nani
Mtani Jembe 2 ambayo imeendeshwa kwa zaidi ya miezi miwili ikiwapa fursa
mashabiki wa timu hizi kuchangia timu zao kila wanapoburudika na bia ya
Kilimanjaro Premium Lager.
Alisema
Nani Mtani Jembe 2 inahusisha mashabiki wa klabu za Simba na Yanga ambapo
zawadi ya shilingi milioni 100 itatolewa na kugawanywa ifuatavyo.
·
Shilingi Milioni 20 ni zawadi ya mechi ya
Nani Mtani Jembe ambapo timu itakayoshinda itapata sh milioni 15 na timu itakayofungwa
itapata shilingi milioni 5.
·
Kampeni hii inaendeshwa kwa njia ya sms
ambapo mashabiki wanapiga kura kwa njia ya sms na shilingi milioni 80
zimegawanywa kati ya timu hizo mbili ambapo kila timu ilianza na shillingi
milioni 40 kwenye benki maalumu mtandaoni.
![]() |
| Meneja Udhamini wa TBL, George Kavishe |
Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium
Lager, Pamela Kikuli alisema mashabiki wa Simba na Yanga wanaweza kushiriki kwa
kununua bia ya Kilimanjaro Premium
Lager yenye ujazo wa mililita 500 ambapo mteja atabandua ganda la kizibo cha
bia ya Kilimanjaro Premium Lager na kuona namba maalumu. Ataandika jina la timu
yake (SIMBA au YANGA) ikifuatiwa na namba hiyo ya kwenye kizibo ambayo anatuma
kwenda namba 15415 na kwa kufanya hivyo anakuwa amepunguza pesa taslimu
shilingi 10,000 kutoka timu pinzani na kuichangia timu yake.
Kikuli pia
alizikabidhi timu hizo jezi maalumu itakayovaliwa mahususi kwa ajili ya mechi
hiyo na kuwahimiza mashabiki waendelee kuzipigia kura timu zao na kikubwa
kuhakikisha wanafika uwanja wa taifa na kujionea wenyewe pambano hilo ambalo
lazima mshindi apatikane.
Mkurugenzi wa Mashindano wa Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura aliwakaribisha mashabiki na kuwaomba
wajitokeze kwa wingi kwani hivi sasa timu hizo ziko kambini zikijiandaa na
mtanage huo wa kukata na shoka unaotarajiwa kuwa na msisimko mkubwa.
Alitaja viingilio vya mechi hiyo kuwa ni shilingi
30,000 kwa VIP B, 20,000/= VIP C, 15,000/= kwa viti vya rangi ya chungwa
kiingilio kitakuwa ni sh 15,000 huku viti vya bluu na kijani tiketi zikiuzwa kwa
sh. 7,000/=.
Wambura alisema pambano hilo litakalosimamiwa na TFF
litaanza saa kumi kamili na litachezwa kwa dakika 90 tu ambapo kama muda huo
timu hizo hazitafungana basi mikwaju ya penati itapigwa ili mshindi apatikane.
Taji la
Nani Mtani Jembe linashikiliwa na Simba ambao waliwafunga mahasimu wao 3-1
katika mechi iliyochezwa Disemba 21, 2013.
Mwisho.








Post a Comment