KLABU ya Kilimanjaro FC ya Pasua, inayocheza ligi daraja la tatu ngazi
ya mkoa wa Kilimanjaro, imepiga hatua moja mbele katika harakati zake
za kutwaa ubingwa wa mkoa wa Kilimanjaro kwa kuifunga Afro Boys ya
majengo, goli 1-0.
Goli la Kilimanjaro FC katika mchezo huo mkali wa raundi ya pili,
hatua ya sita bora, uliopigwa juzi kwenye uwanja wa Ushirika, mjini
Moshi, lilipatinana katika dakika 48, kipindi cha pili, likifungwa na
Jackson Obadia "Messi" kwa shuti kali, akiunganisha pasi ya Ayubu
Lipati.
Kwa ushindi huo sasa, Kilimanjaro FC, maarufu Mpira Pesa, inahitaji
kushinda mchezo mmoja tu kati ya michezo yake miwili iliyosalia ili
kutangazwa bingwa wa msimu 2014/2015.
Mpaka sasa timu hiyo, imeshajikusanyia Pointi 19, ambapo inahitaji
mchezo mmoja mmoja tu kati yake na Polisi Kilimanjaro, utakaopigwa
siku ya Ijumaa, ambao utaifanya ifikishe pointi 22 ambazo hamna timu
yoyote inayoweza kufikisha.
Msimamo wa ligi hiyo unaotarajiwa kumalizika, Februari mosi mwaka huu,
unaonesha kuwa Kilimanjaro FC inaongoza kwa pointi 19, ikifuatiwa na
Hai City, yenye pointi 15 sawa na Afro Boys, iliyoko katika nafasi ya
tatu, zikizidiana kwa tofauti ya magoli.
Nafasi ya nne ni Polisi Mwanga yenye pointi 13 na mchezo mmoja
mkononi, nafasi ya tano ni Polisi Kilimanjaro yenye pointi 4 huku
Sango FC isiyokuwa na Pointi hata moja ikiridhika na nafasi ya mwisho.
Mwisho.
Post a Comment