Na Mwandishi wetu,Dar es salaam
Kamati ya Nidhamu ya
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imetoa adhabu kwa watu tisa
wakiwemo viongozi, wachezaji na kocha mmoja kwa kupatikana na hatia ya makosa
ya kinidhamu.
Katika kikao chake
kilichofanyika juzi (Februari 3 mwaka huu) jijini Dar es Salaam, Kamati hiyo
imewafungia mwaka mmoja viongozi wawili wa Chama cha Mpira wa Miguu wa Wanawake
Tanzania (TWFA) Mkoa wa Mwanza kwa kuwashawishi wachezaji wa Mwanza Queens
kugomea uamuzi halali.
Sophia Tigalyoma
(Mwenyekiti) na Katibu wake Hawa Bajanguo walitiwa hatiani kwa kuwashawishi
wachezaji kugomea uamuzi wa Kamati ya Mpira wa Miguu wa Wanawake ya TFF kutupa
rufani yao dhidi ya Kigoma.
Kocha wa Polisi Tabora,
Eliakim Christopher amefungiwa mechi kumi na kupigwa faini ya sh. 300,000 kwa
mujibu wa Kanuni ya 39(2) ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) baada ya kutiwa
hatiani kwa kumtukana refa wakati wa mechi kati ya timu yake na Panone FC
iliyochezwa mjini Moshi.
Wachezaji wa JKT Oljoro
FC, Dihe Makonga, Swaleh Idd Hussein, Ramadhan Mnyambegu na nahodha Shaibu
Nayopa wamefungiwa mechi tatu na faini ya sh. 300,000 kila mmoja kwa kuzingatia
kanuni ya 36(10) ya FDL kutokana na kufanya vurugu kwenye mechi kati yao na
Burkina Faso iliyochezwa mjini Morogoro.
Mtunza Vifaa (Kit Man)
wa JKT Oljoro FC, Eliud Mjarifu amefungiwa miezi sita na kupigwa faini ya sh.
200,000 kwa kumpiga Kocha wa Burkina Faso, CR Mwakambaya kwenye mechi kati ya
timu hizo iliyofanyika Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
Pia Mjarifu amepewa onyo
kali na kutakiwa kutorudia tena kutenda kosa, kwani hata mwenendo wake wakati
wa shauri hilo ulionyesha utovu wa nidhamu mbele ya Kamati.
Naye Mtunza Vifaa wa
Rhino Rangers FC, Albert Mbuji amefungiwa miezi sita na faini ya sh. 200,000
kwa kupatikana na hatia ya kuwatukana na kugomea uamuzi wa marefa kwenye mechi
dhidi ya Polisi Dodoma. Adhabu hizo zimetolewa kwa mujibu wa kanuni ya 40(2) ya
FDL.
Kamati hiyo imeondoa malalamiko
dhidi ya Ofisa Habari wa klabu ya Ruvu Shooting, Masau Bwire kwa vile refa
Israel Mujuni Nkongo ambaye ni mlalamikaji hakufika kwenye shauri hilo.
Nkongo alimlalamikia
Bwire akidai alitoa maneno yenye kuweza kuchochea chuki dhidi yake kwa waamuzi,
kwani kupitia redio 100.5 Times FM, Bwire alidai refa huyo ndiye aliyeshinikiza
kuondolewa kwa refa Mohamed Theofil kwenye ratiba ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL).
Pia Kamati hiyo imemkuta
bila hatia Kaimu Katibu Mkuu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Singida
(SIREFA), Gabriel Gunda ambaye TFF ilimlalamikia kuwa akiwa mtendaji mkuu wa
chama hicho alishindwa kuhakikisha timu ya Singida inaingia uwanjani kucheza na
Dodoma kwenye mechi ya Kombe la Taifa kwa Wanawake.
Kamati ilikubaliana na
utetezi wa Gunda kuwa, jukumu la timu hiyo lilikuwa mikononi mwa viongozi wa
TWFA Singida, na tayari SIREFA kupitia Kamati yake ya Nidhamu ilishatoa adhabu
kwa viongozi wa timu hiyo kutokana na kitendo hicho.
Nayo malalamiko ya
Polisi Tabora FC kutaka mechi yao dhidi ya Toto Africans FC irudiwe kwenye
uwanja huru (neutral ground) kwa madai ya kuchezeshwa zaidi ya muda unaotakiwa,
na kutokuwepo ulinzi wa kutosha kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza
yamekataliwa.
Pia Kamati ya Nidhamu
imeelekeza malalamiko ya timu za Mwadui FC na Polisi Mara FC dhidi ya Toto
Africans kwa kumchezesha mchezaji Ladislaus Mbogo bila kuonyesha leseni yake
yasikilizwe haraka na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) kwa vile si ya
kinidhamu.
Wakati huo huo, Kamati
ya Nidhamu inaendelea na kikao chake leo (Februari 5 mwaka huu) kusikiliza
malalamiko mengine ya kinidhamu yaliyofikishwa mbele yake.







Post a Comment