Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Ndugu na jamaa wakiwa nyumbani kwa marehemu Bahati Mwanguku ambaye alikuwa afisa Mtendaji wa kijiji cha Mpona Malangali Kata ya Totowe Wilayani Chunya Mkoani Mbeya aliyeuwawa na watu wanadhaniwa kuwa ni majambazi usiku wa kuamkia leo March 3  kijijini hapo.
Mwili wa marehemu Mwanguku ukiwa umefunikwa huku ndugu wa marehemu wakiwa na majonzi kufuatia tukio hilo la kuuwawa kwa Afisa mtendaji huyo kikatili na watu wasio julikana.Picha na Ezekeil Kamanga

Marehemu enzi za uhai wake
Shuhuda wa tukio hilo Huruma simkufukwe


Na Ezekiel Kamanga,Mbeya

Afisa mtendaji wa Kijiji cha Mpona Marangali kata ya totowe Wilayani Chunya Mkoani Mbeya Ndugu Bahati Mwanguku ameuwawa kwa kukatwakatwa na mapanga na watu wanao dhaniwa kuwa ni majambazi usiku wa kuamkia leo March 3 mwaka huu.


Tukio la kikatili limetokea kijijni hapo March 3 mwaka huu majira ya saa 9 usiku ambapo inadaiwa kuwa watu hao  wasiofahamika walifika nyumbani kwa Afisa mtendaji huyo kwa lengo la kuomba msaada .


Mmoja wa ndugu wa marehemu huyo Bw. Huruma Simfukwe alisema kuwa watu hao walifika nyumbani hapo majira ya saa 8 usiku wakitaka kupatiwa msaada kwa afisa mtendaji huyo.


Amesema  marehemu alikuwa amelala nyumba kubwa akiwa yeye na watoto wake ambapo mke alikuwa ameondoka muda mchache kabla ya mauaji hayo akielekea jijini mbeya .


Amesema yeye pamoja na mwenzake walikuwa nyumba ndogo za uwani ambapo walisikia watu wakigonga huku wakimtaka Afisa mtendaji huyo kufungua mlango ili waweze kueleza shida zao.


Amesema marehemu aligoma kufungua mlango huku akiwataka kujitambulisha na kueleza shida zao ambapo walidai wao wametoka usangu Mbarali  hivyo  wanahitaji msaada kwani mifugo yao imevamiwa na majambazi hiyvo wanahitaji msaada wa ulinzi .


Amesema pamoja nakwamba ulikuwa usiku wa manane waliweza kuwaona watuhumiwa hao nakwamba hawakuweza kutambua kitu chochote walichokuwa wameshika tofauti na tochi ambayo ndio waliyokuwa wakiitumia kumulikia .


Amesema mara baada ya watu hao kujieleza afisa mtendaji huyo ambaye kwa sasa ni marehemu aliwataka kurudi kesho yake saa2 asubuhi (Leo  ) ili awapatie msaada huo ambapo watu hao waligoma na kushinikiza marehemu atoke nje  .


Amesema wakati majibizano hayo yakiendelea kati ya marehemu na watuhumiwa hao ghafla alisikia kishindo na kelele zikitoka ndani ya nyumba kama mtu akiomba msaada ambapo kwa muda huo naye alifatwa hadi chumbani alipo lala na watu hao  kisha kufunikwa shuka usoni na kuingizwa chini ya vungu mwa makochi na kutakiwa kukaa kimya.


Amesema wakati matukio hayo yakiendelea alisikia mlio wa pikipiki ikiwashwa kutoka nyumbani hapo na kutokomea pasipo julikana hali ambayo ilimfanya aamke ndipo alipo kutana na damu nyingi zikiwa zimetapakaa chumba kizima huku marehemu akiwa amekatwa katwa mapanga sehemu mbalimbali za mwili wake akiwa tayari amekufa huku pikipiki ya marehemu nayo ikiwa imechuliwa na watu hao .


Hata hivyo Mwenyekiti wa kijiji hicho Pukisaida Mwalobe amesema yeye aliamshwa nyumbani kwake majira ya saa kumi usiku  na mjumbe wa serikali ya kijiji hicho kwa kuelezwa kuwa Afisa mtendaji wake ameuwawa na majambazi.


Amesema mara baada ya kufika nyumbani kwa marehemu alielezwa kuwa kabla ya  marehemu kukutwa na umauti huo ni muda mchache  mara baada ya kutoka  kumsindikiza mke wake usiku huo  ambaye  alikuwa akisafiri kuelekea Jijini Mbeya.


Amesema tukio hilo limewasikitisha sana kwani walipanga kukutana na marehemu huyo ili kupanga mikakati mbalimbali namna ya kuongoza serikali hiyo ya kijiji hicho hivyo kifo cha afisa mtendaji huyo   ni pigo kubwa kwake na kwa serikali ya kijiji kwa ujumla.


Aidha kufuatia tukio hilo ameomba ushirikiano kwa wananchi wa kijiji hicho kuhakikisha wanatoa taarifa kwa uongozi wa kijiji juu watu wanaoingia ndani ya kijiji hicho ili waweze kuwatambua mara moja kwa lengo la kuepuka vitendo vya namna hiyo .


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Ahmed Msangi amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba jeshi la Polisi litahakikisha linawatia nguvuni watuhumiwa hao.

Mwisho.

                                                   JAMIIMOJABLOG















Je, Una Habari,Picha,Tangazo,Makala, Ushauri n.k.?Basi Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp 0759 406 070

Post a Comment

 
Top