Na Baraka Kizuguto,Dar es salaam
Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) limetangaza
viingilio vya mchezo wa siku ya jumapili kati ya Simba SC na Young African
utakaofanyika kwenye dimba la Uwanja wa Taifa kuanzia majira ya saa 10 kamili
za jioni.
Mchezo huo utachezeshwa na mwamuzi Martin Saanya kutoka
Morogoro, akisaidiwa na Soud Lila (DSM) mshika
kibendera wa kwanza, Florentina Zabron (Dodoma) mshika kibendera wa
pili, Mwamuzi wa akiba Israel Mjuni (DSM), na kamisaa wa mchezo ni Ame
Santimeya (DSM).
Viingilio vya mchezo huo, VIP A sh. 40,000, VIP B sh. 30,000, VIP C sh.
20,000, Rangi ya Machungwa (Orange) sh. 10,000, huku Rangi ya Bluu na Kijani
ikiwa ni sh. 7,000.
Tiketi zitaanza kuuzwa keso (jumamosi) saa 2 kamili asubuhi
katika vituo vya, Karume (Ofisi za TFF),
Mgahawa wa Steers (Posta Mpya), Oilcom (Buguruni), BigBon (Kariakoo), Olicom (Ubungo), Dar Live (Mbagala), Uwanja
wa Uhuru, Kivukoni (Ferry) na Makumbusho (kituo cha mabasi).
Magari yenye vibali maalum ndiyo yatakayoruhusiwa kuingia
ndani ya uwanja siku ya jumapili kwa kupitia barabara ya Mandela na Uwanja wa
Uhuru, barabara ya Chang'ombe itafungwa kuanzia saa 12 kamili asubuhi.
TFF inawaomba, wapenzi, washabiki na wadau wa mchezo kununua
tiketi katika vituo vilivyotajwa ili kuepuka kuuziwa tiketi bandia, ili
kuimarisha ulinzi na usalama wa mchezo, mashabiki wenye mabegi, silaha, vilevi
na chupa za maji hawataruhusiwa kuingia navyo uwanjani.
Aidha katika mchezo huo TFF itatoa ujumbe maalum kupitia kwa
wachezaji kuhamasisha juhudi za Taifa za kuzuia mauaji dhidi ya watu wenye
ulemavu wa ngozi (Albino).
Post a Comment